NDIVYO SIVYO: Mvua ikipungua huwa ‘imepusa’ na ikipitiliza huwa 'imeshitadi'
Na ENOCK NYARIKI
SEHEMU nyingi za taifa la Kenya zinaendelea kupokea mvua kwa wingi.
Mvua inapokunya mfululizo usiku kucha au mchana kutwa, watu husema kuwa mvua imezidi, imeongezeka au imenyesha sana. Inapotulia kwa muda, husema kwamba mvua imeacha kunyesha.
Hakika hizi ndizo kauli mbili ambazo ningependa kuziangazia katika makala ya leo. Sisemi kwamba kauli zenyewe zina kasoro yoyote, hapana.
Hakika ujumbe ambao wazungumzaji hudhamiria kuuwasilisha huifikia ‘hadhira’ yao bila tatizo. Lugha ya ‘barabarani’ pia huwa na kusudi lilo hilo – kuuwasilisha ujumbe kwa hadhira lengwa. Hata hivyo, unapozipima kauli hizi mbili utaona kuwa zina mzunguko na kujirudia kwa aina fulani. Mathalani, mtu anapoeleza kitendo cha mvua kutulia kwa muda fulani atashurutika kutumia maneno ‘mvua’, ‘acha’ na ‘kunya’ – isivyo lazima.
Taaluma yoyote huwa na maneno ambayo huteuliwa kwa makini ili kuwasilisha ujumbe moja kwa moja bila kujikita kwenye mizunguko. Kwa hivyo, mvua inapoacha kunya, tunasema imepusa. Matumizi ya neno pusa yatamsaidia mzungumzaji kutolirudia neno kunya au kunyesha.
Baadhi ya kamusi zinaonesha kuwa neno pusa ni kisawe cha anuka. Hata hivyo, kuna mambo mawili yanayoyafanya maneno hayo kutokuwa na usawe wa mia fil mia. Kwanza, neno anuka, lina maelezo ya ziada ambayo hayajitokezi kwenye neno pusa. Kamusi ya Kiswahili- Kiingereza inaeleza kuwa anuka ‘is to stop raining and to be clear again’. Pili, neno anuka linapotumiwa kwa maana ya kuacha kunyesha, husaidia pakubwa katika kuleta iktisadi. Nimeitumia dhana ‘iktisadi’ kwa maana ya matumizi ya maneno machache kuwasilisha ujumbe fulani. Sentensi zifuatazo zitasaidia katika kuifafanua hoja hii:
Tazama mvua imepusa!
Tazama kumeanuka!
Waama, si sahihi kusema “*mvua imeanuka!’’ kwa sababu neno hilo halitumiwi tu kuelezea kupusa kwa mvua bali pia kutoweka kwa utusitusi(gizagiza ) unaoandamana na hali hiyo.
Mvua inapoendelea kunya kwa nguvu bila kukoma, tunasema mvua imeshitadi. Msemo kushitadi pia unaweza kutumiwa kimtambuko kuibua maana nyingine. Kwanza, ni kuendelea kufanyika kwa jambo kwa muda mrefu bila kusimama au kupungua. Pili, ni kuzidi au kukithiri. Mfano: Tabia yake ya wizi wa kimabavu imeshitadi.
Alhasili, mvua inapotulia kwa muda, tunasema imepusa au kumeanuka. Inapokunya kwa nguvu tunasema mvua imeshitadi. Jua linapopoa hususan wakati wa alasiri tunasema ‘jua limepunga’. Kivumishi shadidi hutumiwa kueleza ukali wa kitu au jambo. Mathalani tunasema: Leo kuna baridi/jua shadidi.