Nema yaamuru KPC kusafisha upya mazingira yaliyochafuliwa na mafuta
MAMLAKA ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) imebatilisha agizo la mwaka 2018 lililosema kuwa mto Thange ulioko Kaunti ya Makueni ulikuwa safi baada ya kuchafuliwa na mafuta.
Jana, mamlaka hiyo ilithibitisha kuwa udongo na vyanzo vya maji katika eneo hilo bado vinachafuliwa na mafuta.
NEMA iliamuru Kampuni ya Mabomba ya Mafuta ya Kenya (KPC) kuanza tena mchakato wa kusafisha mazingira yaliyochafuliwa na mafuta kutokana na bomba lililovuja mwaka 2015.
“Wananchi wana haki ya kuishi katika mazingira safi. Kuanzia Jumatatu tutapitia upya agizo la kurejesha mazingira ili KPC ishughulikie usafi kwa mujibu wa sheria. Hatutaruhusu wananchi kutumia mazingira haya kwa hali ilivyo sasa,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NEMA Boru Mano, alipokuwa akizungumza na wanahabari wakati wa ziara ya eneo hilo akiwa na Kamati ya Seneti kuhusu Nishati na viongozi wa eneo hilo.
Seneta Oburu Odinga, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Seneti, alisema kuwa walilazimisha NEMA kuchukua hatua upya dhidi ya KPC ili kurejesha mazingira yaliyoharibiwa.
Ziara hiyo ilijiri baada ya malalamishi kuongezeka kufuatia ripoti za vifo na maambukizi ya maradhi ya ini na figo. Ripoti za kitabibu zilizoonekana na Taifa Leo zinaonyesha maradhi hayo yanahusishwa moja kwa moja na uchafuzi wa mafuta.
Mwakilishi wa Wadi ya Thange Eric Katumo ndiye aliyeanzisha juhudi za kupata taarifa kutoka kwa Kamati ya Mazingira ya Bunge la Kaunti ya Makueni, na kuandikia KPC na NEMA akiomba msaada wa haraka.
Aliungwa mkono na Gavana Mutula Kilonzo Junior, Seneta Daniel Maanzo na Mbunge wa Kibwezi Mashariki Jessica Mbalu, waliotaka usafi huo ufanyike upya pamoja na fidia kwa waathiriwa.
Ripoti ya athari za kijamii na kiuchumi iliyotayarishwa na Panafcon Consultants Ltd, waliokodiwa na KPC, inaonyesha hali mbaya ya eneo hilo ambalo zamani lilijulikana kwa kilimo cha mboga.
Kati ya wakazi 1,071 waliopimwa, 161 waligunduliwa kuugua kutokana na sumu za kemikali zinazopatikana kwenye mafuta.
Mwalimu Edward Muia, aliyekuwa mmoja wa waathiriwa alifariki dunia kutokana na maradhi ya ini na figo.
Katika tukio la kushangaza, Seneta Oburu alishuhudia kwa mshtuko timu ya Gavana Kilonzo Jr ilipogundua mafuta katika visima vitatu vipya vilivyochimbwa eneo hilo.
Alisema ripoti nyingi rasmi zinaonyesha athari kubwa za kiafya na kiuchumi kwa jamii ya Thange, na akaitaka KPC iwajibike.
Katika barua iliyoandikwa Aprili 30 2025 kwa Kamati ya Seneti kuhusu Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa KPC Joe Sang alidai kuwa kampuni hiyo ilitekeleza usafi wa kutosha eneo hilo baada ya ajali ya 2015, na kwamba NEMA iliwapa kibali cha kusitisha shughuli mnamo Februari 2018 na Julai 2021.
Pia alifichua kuwa jumla ya familia 342 zilipokea Sh38 milioni kama fidia kutoka KPC.
Lakini Seneta mteule Beatrice Ogola alisema,“Tusikatae yaliyotokea hapa. Mashirika ya serikali lazima yawajibike. KPC lazima itekeleze wajibu wake. Sio fidia tu kwa mali iliyoathirika, bali ni kuhusu afya ya watu hawa. Miaka michache ijayo jamii hii inaweza kutoweka.”