NGILA: Blockchain itasadia pakubwa kuzima corona
Na FAUSTINE NGILA
NILIPOSOMA mitandaoni kuwa China ilikuwa imeuza vifaa bandia vya kupimia virusi vya corona vipatao 640,000 kwa taifa la Uhispania, nilifikiri ni habari feki tu kama ilivyo desturi ya mitandaoni enzi hizi.
Lakini gazeti la New York Times lilipochapisha kuwa kampuni moja nchini China imejitolea kutuma vifaa vingine halisi ili kufidia Uhispania vile vya awali, niliamini habari hizo.
Niliishangaa China, kwa uwezo wake wote wa kiteknolojia mbona imeshindwa kuunda mfumo wa teknolojia ya Blockchain kubaini vifaa vilivyoidhinishwa na vile bandia.
Hata hivyo, nimefurahishwa na Shirika la Afya Duniani, kwa ushirikiano wake wa hivi karibuni na kampuni za teknolojia za IBM na Oracle kwa uvumbuzi wao hivi majuzi wa mfumo wa blockchain wa kuidhinisha data kuhusu gonjwa la corona.
Mfumo huo kwa jina MiPasa, unatarajiwa kubadilisha jinsi ugonjwa huo unakabiliwa, kwa kutumia teknolojia za kuchanganua data ya kijiografia ili kubaini maambukizi mapya katika maeneo mengi duniani.
Kwa hakika, hasa mataifa yanayoendelea kama Kenya, hakuna data ya kutosha ya kusaidia kufanya maamuzi ya dharura.
Serikali ya Uingereza, kwa mfano, imeshirikiana na kampuni ya mawasiliano ya simu ya O2 kutumia data kuhusu raia wake kuwaonya dhidi ya kutoka nje ya nyumba kila mara. Kwa wanaotokatoka nje, wanapigwa faini kwa mishahara yao.
Wakenya, ambao wameonyesha ukaidi katika kufuata maagizo ya serikali kuhusu kuzuia maambukizi mapya ya virusi hivi, inahitaji mfumo kama huo ili kuwatambua wanaokiuka sheria na kuwatumia ujumbe moja kwa moja.
Blockchain ni teknolojia ambayo tayari imeshuhudia ufanisi katika kuzima maovu katika uchumi, na suala la kuuziwa vifaa feki vya kupima ugonjwa, dawa feki, barakoa feki au bidhaa zozote za kiafya bandia, laweza kuzimwa.
Kwa kushirikisha programu za kufuatilia na kuchambua data ya simu, Blockchain itakuwa ya msaada sana katika kipindi hiki cha kuenea kwa virusi vya corona, kwani kupitia mfumo wake, serikali itakuwa na kazi rahisi kufuatilia watu waliotangamana na mgonjwa wa virusi hivi.
Kwa kuwa Kenya inajivunia kuwa na jopokazi la blockchain, serikali inafaa kuwa mbioni kubuni mfumo wa kiteknolojia kuunganisha data za simu na afya za watu wote wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo, kisha kufuatilia hali yao ya kiafya.
Vipimo vya joto, kikohozi na ukosefu wa hewa ya kupumua vyafaa kuwa vigezo muhimu katika kung’amua hali ya wagonjwa, na hii pia inaweza kutumiwa kubashiri idadi ya watu wanaoweza kupatikana na ugonjwa huo katika miezi ijayo.
Nimeona baadhi ya mataifa duniani yakidinda kutoa taarifa kuhusu idadi kamili ya watu waliougua, na hiyo ni tisho kubwa katika kuuelewa ugonjwa huu ulioangamiza watu zaidi ya 30,000.
Hivyo, ni muhimu kwa mataifa yote kushirikiana na kutumia teknolojia hizi ili kupunguza maambukizi mapya. Ni kupitia njia hii ambapo uchumi wa dunia ambao umezama ramsi kwa sasa, utaweza kunyanyuliwa maambukizi yakizimwa.