NGILA: Kenya si mfano bora wa ufanisi wa teknolojia Afrika
NA FAUSTIN NGILA
WITO wa Rais Uhuru Kenyatta wiki iliyopita nchini Rwanda kwa nchi za Afrika kuupa kipaumbele ushirikishi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika mipango yao ya maendeleo, unajiri wakati mwafaka ambapo uchumi wa bara hili unahitaji mbinu mbadala kuuimarisha.
Katika uzinduzi wa mpango unaolenga kubuni soko la pamoja la kidijitali katika bara hili ili kufanikisha biashara na uwekezaji nchini Rwanda, Kenya iliibuka kuwa na mpango bora wa kuimarisha uchumi wa Afrika.
Hata hivyo, kama mwandishi na mtafiti wa masuala ya teknolojia, ninafahamu kwamba licha ya Kenya kuwa kifua mbele katika uelewaji na utekelezaji wa miradi tajika ya dijitali, bado kuna changamoto nyingi nchini ambazo zinatulemaza kufikia uwezo wa mataifa kama Amerika, Uchina na Japan.
Mkakati wa kidijitali wa Kenya chini ya mada: Kuthibiti Uwezo wa Mabadiliko nchini Kenya uliozinduliwa mbele ya zaidi ya wajumbe 4,000 miongoni mwao maafisa wa serikali, watunga sera, wabunifu na wawekezaji, ulitumiwa kujadili jinsi teknlojia inaweza kulifaa bara hili kibiashara.
Kile ambacho Rais hakuwaambia wajumbe hao ni kwamba mazingira yetu ya teknolojia si mazuri vile, licha ya kampuni nyingi za teknolojia kutoka ng’ambo kupendelea kuwekeza jijini Nairobi kutokana na taswira ya ukumbatiaji mzuri wa teknolojia miongoni mwa vijana.
Ikiwa mataifa ya Afrika kwa kweli yanakusudia kuimarisha mchango wa teknolojia ya habari na mawasiliano kwa uchumi, basi yanafaa kutumia mifano ya miradi tajika duniani kama ‘Silicon Valley’ ya Amerika.
Kutumia ‘Silicon Savannah’ ya Kenya kama mfano bora ni sawa na kutumia ‘Yabacon Valley’ ya Nigeria kama kielelezo. Mataifa yote mawili yanakumbwa na changamoto za ukuaji wa teknolojia, licha ya kujigamba kuwa mabingwa wa matumizi ya mitambo ya kidijitali barani.
Kwa kawaida, mataifa ya Afrika husalia nyuma wakati maendeleo na mageuzi muhimu ya teknolojia yanafanyika kote ulimwenguni. Kwa mfano, hadi kufikia sasa, gharama ya intaneti iko juu zaidi hapa barani ikilinganishwa na mabara mengine.
Wakati umefika kwa viongozi wa mataifa ya Afrika kuipa teknolojia nafasi kubwa kwa kuboresha miundombinu kama kuondoa ushuru kwa vifushi vya data ya intaneti na mawasiliano ya simu.
Pia michakato ya kusajili kampuni za teknolojia yafaa kulainishwa, elimu ya dijitali ienezwe na kutenga fedha za kutosha kwa utafiti na sayansi.
Vijana wa Afrika pia wanahitaji kugutuka na kujifunza kupambana na vizingiti hivi.