NGILA: Kilio cha Zuckerberg ishara ya uzembe wa Facebook
NA FAUSTINE NGILA
KILIO cha mwasisi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg kwamba serikali zote duniani zinafaa kumsaidia kukabiliana na jumbe, picha na video hatari kwa jamii kinachekesha.
Akilalamika wiki iliyopita, Zuckerberg, ambaye ndiye Afisa Mkuu Mtendaji wa Facebook, alidai kuwa jukumu hilo ni nzito mno kuachiwa kampuni chache.
Aliyaomba mabunge ya serikali zote duniani kumsaidia kutokomeza taarifa zisizofaa mtandaoni, kuhakikisha kuna maadili na kuwahakikishia watumizi usiri wa data.
Ikumbukwe kuwa mtandao huu umekuwa ukitumika hata na magaidi kupeperusha video za wakiua watu, mfano ukiwa tukio la mauaji katika msikiti wa Chirstchurch, New Zealand.
Lakini kilio cha Zuckerberg ni mzaha mkubwa katika sekta ya teknolojia duniani. Iweje uunde mtandao ambao unakulemea kudhibiti?
Tayari kampuni yake ina kila taarifa, data, vifaa na wataalamu ambao wanafaa kudhibiti mtandao huo bila kuomba msaada wa sheria za mataifa binafsi.
Kila taifa tayari lina sheria za kudhibiti mawasiliano, lakini utekelezaji wa sheria hizo hauwezi kuzuia maafa ya moja kwa moja kama shambulio la New Zealand.
Kampuni ya Facebook inaonyesha uzembe katika kukabili maovu mitandaoni, maanake ina teknolojia zote za kukusanya data moja kwa moja na kung’amua wakati kuna majanga.
Utaona ujumbe wa Facebook wa kuwaomba watumizi wake ‘wajitie alama kuwa wako salama’ wakati wa mafuriko na vimbunga. Iweje iwe vigumu kuwaarifu watumizi wa eneo ambalo ugaidi unafanyika na unarekodiwa kupitia kwa mtandao wao? Mbona wasiarifu polisi kwa wakati unaofaa.
Facebook inajitia hamnazo. Inajifanya haina uhuru wa kuzuia usambazaji wa video za mauaji.
Kuhusu uchaguzi, kampuni hii imekuwa lawamani kwa kutumiwa na makundi ya kisiasa kuwachafulia majina washindani. Kila mwaka, inajua mataifa ambayo yanaandaa uchaguzi mkuu, mbona isijitayarishe kwa uchaguzi na kuzuia jumbe za chuki na propaganda za kugeuza maamuzi ya wapigakura?
Kampuni hii ina majina yote ya makundi ya kisiasa kwenye mtandao wake, hivyo ina data yote katika lugha tofauti. Mbona isiwekeze kukuza demokrasia. Matrilioni ya faida inayopata yanatumika kufanya nini?
Tayari mamilioni ya watu duniani wamefuta akaunti zao kwenye mtandao huo kutokana na uzembe wake wa kuzuia udukuzi na usambazaji wa data za siri.
Zuckerberg akome kujifanya limbukeni wa teknolojia, achuke hatua zifaazo kuziba ufa huu. Gharama ya kujenga ukuta itakuwa juu zaidi na jamii zijazo zitashangaa kusikia kulikuwa na mtandao ulioitwa Facebook.