• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
NGILA: KRA isikubali biashara za mitandaoni zikwepe ushuru

NGILA: KRA isikubali biashara za mitandaoni zikwepe ushuru

NA FAUSTINE NGILA

HUKU mizizi ya teknolojia ikizidi kupenyeza katika uchumi wa Kenya, biashara za mitandaoni zimeongezeka kwa kasi mno katika miaka minne iliyopita.

Wakenya wengi hupendelea kulipia bidhaa na huduma kupitia majukwaa ya kidijitali, lakini kuna ufa mmoja ambao unatisha kuinyima serikali mapato.

Ukosefu wa sheria na sera mwafaka katika mchakato mzima wa kukusanya ushuru kutokana na biashara za mitandaoni ni pengo ambamo mabilioni ya ushuru hupotelea.

Mojawapo ya nguzo kuu katika ukusanyaji wa ushuru ni ushirikishi na usawa, ambapo kila mja anatakiwa kisheria kulipa ushuru kulingana na mapato yake. Hii husaidia katika ugavi sawa wa utajiri wa nchi.

Ingawa ninakiri kuwa bishara za intaneti zimesaidia kupiga jeki uchumi, uwezo wa uchumi hauwezi kutambulika iwapo biashara hizi zitazidi kuruhusiwa kukwepa kulipa ushuru.

Mabilioni ya pesa yametumwa na kupokelewa kupita mifumo ya dijitali. Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA) imekadiria sekta ya biashara za mitandaoni kuwa na thamani ya Sh4.3 bilioni. Nayo biashara ya kuuza na kununua sarafu za kidijitali kama Bitcoin nchini ina thamani ya Sh150 bilioni.

Hizi tu ni takwimu za sehemu ndogo ya sekta nzima ya kutengeneza mkwanja mitandaoni, ukizingatia mauzo mengi hufanyika kupitia Jumia, Kilimall, Amazon, e-Bay, Facebook, Twitter, Instagram miongoni mwa majikwa mengine.

Licha ya maelfu nafasi za kazi kuundwa Kenya kutokana na huduma za kuandika habari na makala mitandaoni, waandishi hawa hawalipi ushuru. Wao hutumia mitandao ya kimataifa kupokea malipo kama Paypal, Payoneer, Due, Stripe, Skrill, Pesapal na iPay ambayo inafaa kushirikiana na serikali na kuwakata ushuru.

Hata hivyo, kuna changamoto. Biashara za mitandaoni hazina anwani za mahali zinapofanyia kazi na hivyo imekuwa vigumu kukwepa kulipa ushuru.

Kenya, kama mataifa mengine kama Afrika Kusini, India, Philippines, Israel, Japan, Thailand na Ufaransa inafaa kuanza kukabili changamoto hizi.

Sehemu ya Tatu katika Sheria ya Ushuru nchini inatoza ushuru mapato ya kila mtu anayopata kutokana na mazingira ya biashara ya Kenya, awe Mkenya au raia wa kigeni.

Mswada wa Fedha 2019 umependekeza mageuzi katika utozaji wa ushuru, kushirikisha masoko ya mitandaoni kuhakikisha mauzo yote ya kidijitali yamekatwa ushuru kulingana na sheria.

Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA), Wizara ya ICT na Hazina Kuu zinafaa kushirikiana kuhakikisha mazingira ya kukusanya ushuru yameboreshwa na bishara zote za mitandaoni kupewa leseni.

Ni hatua kama hii ambayo itasaidia serikali kukoma kutegemea misaada ya kifedha kutoka nje na kupunguza kiwango cha ukopaji wa mabilioni. Mwanzoni kutakuwa na visiki, lakini hatimaye tutaona matunda ya juhudi hizi. Tukilipa ushuru, hakika tutajitegemea kwa mambo mengi.

You can share this post!

Mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni Afrika Kusini yaushtua...

ONYANGO: Isiwe Mau pekee, wote wanaoishi misituni watoke

adminleo