Makala

NGILA: Mawimbi ya 4G yatasaidia kupunguza bei ya simu

August 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA FAUSTINE NGILA

Mwezi uliopita, nilihudhuria uzinduzi wa intaneti ya kasi ya kisasa inayotumia mawimbi ya 4G katika eneo la Mogotio, Kaunti ya Baringo ambapo Kenya iliweka historia duniani.

Nchi hii sasa ni ya kwanza kabisa kutumia mawimbi hayo kibiashara.Kupitia Telkom Kenya na kampuni ya Google, wakazi wa kaunti 14 eneo la Bonde la Ufa na Magharibi sasa wanafurahia intaneti ya bei nafuu inayopeperushwa kutoka angani kwa puto (baluni).

Hata hivyo, katika hafla ya hiyo, Waziri wa Teknohama Joe Mucheru alikiri kuwa iwapo kupunguzwa kwa bei ya intaneti kutailetea Kenya manufaa, gharama ya kununua simu pia inafaa kuwa chini.

Kuna haja gani kuwa na intaneti ya kasi ya juu, tena ya bei nafuu, lakini haiwezi kuwafaidi mamilioni ya Wakenya ambao hawawezi kumudu bei ya simu za kisasa ambazo zinasaidia kufanikisha suluhu kwa changamoto za kielimu, kiafya na kibiashara mashinani?

Kana kwamba ilikuwa ikisubiri uzinduzi huo, kampuni ya Safaricom nayo majuma machache yaliyofuata ilizindua mpango wa kuwapa wakazi wa tabaka la chini simu za kisasa kwa kulipa Sh20 pekee kila siku.Kwa sasa, simu ya kisasa ya bei nafuu zaidi hugharimu mteja Sh4,000, lakini kupata hela hizo hasa wakati huu wa janga la corona kumekuwa kama kushuka mchongoma.

Simu zenyewe pia, kwa mfano, hazijatimiza ubora wa kutazama video za mbashara.Ingawa hatimaye simu za Sh20 kwa siku zinauzwa kwa riba ya asilimia 13 na kufikisha bei kamili Sh7,000, zitasaidia pakubwa kupunguza mwanya uliopo baina ya matajiri na makabwela katika ulingo wa teknolojia.

Tunaposema kuwa Kenya imepiga hatua katika masuala ya teknolojia, mara nyingi tumekuwa tukisahau kuwa huduma za kisasa zinatumika tu na asilimia 40 ya Wakenya pekee ambao wana uwezo wa kujinunulia simu za kisasa.

Hivyo, hatua ya kuwepo kwa intaneti katika kila kona ya nchini hii kutafungua nafasi kwa kampuni za kutengeneza simu kushindania soko la Kenya.

Ni ushindani huu ambao utapunguza gharama ya simu hata zaidi kuliko mpango wa sasa wa Safaricom, na huenda ukapata simu nzuri ya kisasa kwa Sh1,000 kufikia mwaka wa 2024.

Iwapo angalau asilimia 80 ya Wakenya watajinunulia simu, basi wakati utakuwa umetimu kwa wanafunzi wote kufundishwa mitandaoni, wagonjwa kutibiwa kupitia kwa simu zao na biashara kuvuma kwenye intaneti.

Ni teknolojia hizi ambazo zitasaidia wafanyabiashara, kampuni na idara za serikali kupunguza gharama za uwekezaji, huku zikivutia wawekezaji kutoka mataifa ya kigeni.