NGILA: Sheria na asasi hasi zinalemaza ustawi kiteknolojia
NA FAUSTINE NGILA
LICHA ya Kenya kusifiwa kwa uwezo wake wa uvumbuzi, bado kuna vizingiti vingi ambavyo vinawazuia vijana kuafikia ndoto zao.
Iwapo unapania kuonja matunda ya uvumbuzi wako, utahitajika kuruka viunzi vingi kama sheria zilizopitwa na wakati, michakato ya kuchosha, ukosefu wa mtaji, washauri bandia na serikali isiyotambua teknolojia.
Hatua 21 zinahitajika kwa wawekezaji kuruhusiwa kuingia kwenye mikataba ya maana na serikali za kaunti. Kutokana na hili, taifa hili linachangia kudidimia kwa uchumi maanake bidhaa na huduma kutokana na teknolojia hatimaye hazifiki sokoni.
Idadi kubwa ya Wakenya husalia bila ajira huku taifa likipoteza mabilioni ya fedha kutokana na sera mbovu za teknolojia.
Sheria ngumu pamoja na michakato ghali ni majabali ambayo serikali imeonekana kutotaka kuyaondoa, na sasa mamia ya wavumbuzi wamesalia na mawazo yao pevu kwa akili zao tu, wakijua fika wakijaribu kuyatekeleza itakuwa sawa na kushuka mchongoma.
Serikali haina budi kuwaondolea wavumbuzi shida wanazopitia. Sheria na kanuni zinazowazuia kuzindua programu za kidijitali zinahitaji kuchunguzwa upya ili kuwapa nafasi kuchangia kukuza uchumi.
Bali na kutambuliwa kuwa nguzo kuu katika kufanikisha Ruwaza ya 2030, sayansi na teknolojia ziko katika sheria za nchi.
Sheria ya Sayansi, Teknolojia na Habari ya 2013 ilibuni asasi nne za kuhakikisha Kenya imepiga hatua kiteknolojia.
Lakini Mfumo wa Kitaifa wa Uvumbuzi (STI), Tume ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi (Nacosti), Hazina ya Kitaifa ya Utafiti (NRF), na Shirika la Kitaifa la Uvumbuzi (Kenia) zimelemewa na kazi.
Wakati umefika kwa Kenia kushirikiana na Nacosti kuunda na kusimamia mfumo wa kitaifa wa uvumbuzi huku ubora ukizingatiwa katika nyanja zote za teknolojia. NRF nayo inafaa kuwa mbioni kusaka fedha kutoka kwa serikali na mashirika ya kimataifa ili kufadhili miradi ya uvumbuzi.
Miaka mitatu tangu Kenia na NRF zibuniwe, bado hakuna lolote zimefanya, licha ya kuwa na wataalamu kwenye bodi zake. Kinaya ni kwamba watu hawa bado wanamumunya mishahara licha ya kutofanya kazi yoyote.
Iwapo serikali haitaondoa changamoto katika asasi hizi, basi ndoto na nia za wavumbuzi kupunguza ukosefu wa kazi na kujenga himaya ya teknolojia Afrika zitazidi kuwa ndoto.