Makala

NGUGI: Tusipoteze dira tufuatiliapo masuala muhimu ya taifa

August 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MWITHIGA NGUGI

WIKI kadha zilizopita tulisikia minong’ono ya sukari hatari iliyoingizwa humu nchini kutoka taifa jirani. Kwa kasi ya paa aliyejeruhiwa na samba, lawama zilianza huku kukionekana bayana vita vya maneno kati ya wabunge na mawaziri viliashiria kulikuwemo na jambo fiche.

Kilichowashangaza wengi ni jinsi ripoti ya kamati ya bunge kuhusu sukari ambayo iliaminika kuwa na madini hatari ilivyozimwa na kukataliwa bungeni.

Baadhi ya wabunge nakumbuka walinukuliwa wakisema kuwa ripoti yenyewe hasa ilikuwa imechakachuliwa huku wengine wakidai kuna waliopokezwa hongo ili kuidonoadonoa ripoti yenyewe na hivyo basi kusalia tu kama mhuri wa kuwatakasa wahalifu, ambao tayari walikuwa wamewaroga Wakenya kwa sukari yenye sumu.

Hata kabla ya vumbi na dhoruba kali ya kuwasaka ‘walanguzi wa sukari’ hazijatulia, Wakenya walitangulizwa tena na ‘filamu’ mpya ya bomoa bomoa za nyumba zinazosemekana zimejengwa karibu na kingo za mito na zingine kwenye maeneo yanayofaa kuwa barabara.

Kwangu mimi sikatai, kujenga kwenye kingo za mito au kwenye maeneo yaliyotengewa barabara ni hatia na ni jambo ambalo kamwe halifai, lakini swali ni je, aliyetoa idhini ya ujenzi kama huu na hata kuwapa wenye majumba kama haya kibali cha kuendelea kujenga yuko wapi?

Sijasahau, wakati Bw Raila Odinga alikuwa waziri wa Barabara, ubomoaji kama huu wa majumba ya kifahari ulishuhudiwa, kwa wakati huo wengi walimuona kama alikuwa akilenga na kuadhibu jamii fulani, jambo hili lilimtia matatani hususan kisiasa.

Lakini hata hivyo ukweli kama ulivyo moshi, haufichiki na ndiposa sasa tunaona majumba ya kifahari yakiporomoshwa na matingatinga bila kusaza. Naamini hili litakuwa ni funzo kwa wote wanaopenda kunyakua ardhi ya umma na wote wakumbuke, siku za mwizi ni arobaine.

Huu si wakati wa kulala ilhali maovu yanaendelea kutendeka, Wakenya sharti wawe macho usiku na mchana kufuatilia masuala muhimu ya taifa yanayowahusu. Bila woga siku zote lazima tuwawajibishe viongozi wetu kwa matendo yao, kwani tusipofanya hivyo tayari tutakuwa tumelisaliti taifa letu na kuumbua uzalendo wetu na kwa upofu kama huu, naamini kizazi cha kesho hakitakuwa na msamaha kwetu.

Ninachoamini kwa sasa ni kuwa Rais wetu Uhuru Kenyatta, amejitoa mhanga kupigana kabisa na wale wote wamekuwa wakijihusisha na uhalifu wa kiuchumi. Alipoapa kuwa yu tayari kuwapoteza hata marafiki, nilijua kwa yakini kuwa huu ndio mwanzo mpya wa kujenga taifa letu.Aliyekula za haramu mwishowe zitamtokea puani.