Makala

Ni nani alimuua dereva wa teksi Victoria Mumbua?

Na KEVIN MUTAI, VALENTINE OBARA, LABAAN SHABAAN October 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DEREVA wa teksi Victoria Mumbua Muloki alifanya kazi hii kwa miaka minne kabla ya kutoweka juma lililopita na kupatikana amefariki Jumatano Oktoba 2, 2024.

Bi Muloki, mwenye umri wa miaka 35, alipotea baada ya kumchukua mteja kutoka Mombasa hadi Samburu, Kaunti ya Kwale Ijumaa iliyopita.

Baadaye, mwili wake ulipatikana katika hifadhi ya maiti ya City jijini Nairobi.

Kulingana na familia, Bi Muloki alianza na kazi ya afisa wa mauzo aliyesafirisha bidhaa za nyumbani kabla ya kuiacha na kuingia katika sekta ya teksi inayotawaliwa na wanaume.

Wafanyakazi wenzake wa Mombasa walifichua kuwa hapo awali alikuwa na gari dogo aina ya Toyota Vitz, kabla ya kuimarika na kununua gari jipya aina ya Nissan Serena lenye nambari ya usajili KDQ 182F.

Tovuti ya Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSA) inaonyesha Bi Muloki si mmiliki wa gari hilo la Nissan Serena.

Limesajiliwa chini ya kampuni ya ENK Enterprises Limited.

Polisi walipata gari hili jijini Nakuru baada ya Bi Muloki kuripotiwa kutoweka.

Maelezo zaidi yanaonyesha kuwa gari hili liliundwa mwaka 2017 na kusajiliwa na NTSA mnamo Mei 30, 2024.

Hii inamaanisha kuwa limehudumu nchini kwa takriban miezi minne.

Kwa sasa, maafisa wa upelelezi wanasaka ushahidi kufichua ni kwa nini mama huyo wa watoto watatu aliuliwa.

Baada ya kutoweka, polisi waliripoti kuwa Bi Mumbua amepatikana akiwa hajielewi Kaunti ya Migori lakini familia yake ikapinga ripoti hiyo.

Mshukiwa alikamatwa

Mshukiwa, Edwin Ngetich Kipkemoi, alikamatwa Jumapili Pipeline Junction katika Barabara kuu ya Nakuru-Nairobi alipokuwa akiendesha gari jeupe aina ya Nissan Serena lenye nambari ya usajili KDQ 182F.

Wanaochuma riziki pamoja naye katika biashara ya teksi wanammiminia sifa kuwa mtu  aliyejitolea na kuthamini kazi yake.

Kulingana na Bw Joe Kairo, mmoja wa madereva wa teksi jijini Mombasa, Bi Mumbua alipenda kuendesha gari na mara nyingi alikubali kuwabeba wateja  kwa mapendekezo ya wenzake.

“Nilimjua kama mtu ambaye alithamini wakati. Hakuwa na ugomvi na mtu yeyote na kila mara alihakikisha kila kitu kinafanyika kwa ukamilifu,” akasema Bw Kairo.

Aliishi na watoto

Bi Muloki aliishi na watoto wake watatu ambao amekuwa akiwalea nyumbani kwao Makupa baada ya kutengana na mumewe.

Familia yake inasema hawana habari ya kina kuhusu kilichosababisha kusambaratika kwa ndoa yake.

“Hajawahi kutofautiana na mtu yeyote. Alitengana na mumewe na tangu wakati huo amekuwa mlezi pekee wa watoto wake watatu. Nijuavyo, hakuna mawasiliano kati yao,” mamake, Bi Anne Kanini alisema katika mahojiano ya awali.

Madereva wa teksi jijini Mombasa waliibua wasiwasi kuhusu visa vya utekaji nyara na unyanyasaji wanaofanyiwa wenzao.

Wanalilia serikali na usimamizi wa teksi zinazotumia apu kuwalinda na kuwahakikishia usalama kazini.