Ni njaa ilipeleka Raila kwa Uhuru, kitabu cha Mudavadi chafichua
JULIUS SIGEI Na BENSON MATHEKA
MATATIZO ya kifedha ni moja ya sababu kuu zilizomfanya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kukubali mwafaka wa maelewano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, maarufu kama handisheki 2018.
Kulingana na Kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi, ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa vigogo wanne wa upinzani waliokuwa mrengo wa NASA, Bw Odinga pia alikuwa na presha kali kutoka mataifa ya kigeni yaliyomtaka kukomesha msimamo mkali kuhusu matokeo ya urais baada ya uchaguzi wa 2017.
Kwenye kitabu chake, “Soaring Above the Storms of Passion”, Bw Mudavadi anasema kulikuwa na kesi nyingi ambazo zilihitaji kiasi kikubwa cha pesa ambazo upinzani haukuwa nazo.
“Tuligundua hatukuwa na uwezo wa kifedha kukabili kesi zilizokuwepo. Ukweli ni kuwa hali ilikuwa mbaya,” asema Bw Mudavadi.
Pia anafichua jinsi Bw Odinga ‘alivyowaacha kwenye mataa’ yeye pamoja na Seneta Moses Wetangula wa Bungoma na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu kiapo alicholishwa na Miguna Miguna mnamo Januari 30, 2018 kuwa “rais wa wananchi”.
Kulingana na Bw Mudavadi, wote wanne walikuwa wamekubaliana kusitisha kiapo hicho kutokana na presha kali walizokuwa nazo kutoka pande tofauti.
Lakini walishtukia kupata habari kuwa Bw Odinga aliwapuuza na kwenda Uhuru Park alikoapishwa na Bw Miguna.
“Makubaliano yetu sote yalikuwa twende Uhuru Park siku hiyo na tuwaambie wafuasi wetu kuwa kiapo kimeahirishwa. Tulikubaliana tukutane asubuhi hiyo na kwenda Uhuru Park Pamoja,” adokeza.
Asubuhi hiyo, asema Bw Mudavadi, wote isipokuwa Bw Odinga walikutana nyumbani kwa Bw Wetang’ula: “Tulipopokea simu yake na alikuwa akizungumza kama mtu ambaye yumo kwenye hatari. Hatungeweza kuelewana. Muda mfupi baadaye tulipata habari alikuwa Uhuru Park akila kiapo.”
Anamtaja Bw Odinga kama mtu asiyeaminika na anayetaka watu wafuate anayotaka yeye, kiongozi ambaye kila mara yuko na mpango mbadala na anayeweza kubadilisha kauli wakati wowote.
Anasema wakati mmoja walipokuwa wakimshawishi kutokula kiapo, walifahamu kwamba Bw Odinga alikuwa nyumbani kwa Jimi Wanjigi akiwa na watu wa familia na wandani wake wakipanga kurekodi akila kiapo kisha itangazwe isambazwe katika vyombo vya habari.
Bw Mudavadi pia anasimulia kuwa Bw Odinga aliwaficha wakuu wenzake katika Nasa kuhusu handisheki.
“Nilikuwa nikielekea Mombasa nilipopokea simu kutoka kwa seneta wa Vihiga, George Khaniri kunifahamisha kuhusu handisheki nje ya Harambee House katika ofisi ya Rais.
“Baada ya hapo nilipokea simu nyingi. Kalonzo alinipigia akitaka kujua ikiwa nilikuwa na habari kuhusu kilichokuwa kikiendelea. Nilimweleza kwamba sikuwa na habari,” anasimulia Bw Mudavadi.
Anasema kuwa alipata presha kutoka kwa watu wa matabaka mbalimbali waliotaka kujua kilichokuwa kikiendelea ikizingatiwa kwamba alisimamia kampeni za urais za Bw Odinga.
“Walitaka kujua iwapo sasa tulikuwa katika serikali ya muungano na Jubilee,” anaeleza. Kiongozi huyo wa chama cha ANC.
Katika mkutano wa vinara wa Nasa uliofanyika Athi River baada ya handisheki, Bw Mudavadi anafichua kuwa joto lilipanda wakitaka Bw Odinga kueleza kwa nini mazungumzo yake na Rais Kenyatta yalikuwa ya siri.
“Kwenye mazungumzo hayo, iliibuka kuwa vikwazo kuhusu viza vilionekana kuwekewa watu wengine wengi,” anasimulia.
Anafichua kuwa katika mkutano mmoja kabla ya handisheki, Bw Odinga aliwaonyesha barua moja aliyoandikiwa na ubalozi wa nchi moja ya Ulaya kufuta viza yake.
Wakati mmoja, anaeleza, Odinga alikaidi ushauri wa aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo.