Makala

Ni uabudu shetani au nini? Maimamu, kina mama Lamu wakemea mauaji ya wanawake nchini

Na KALUME KAZUNGU November 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa dini ya kiislamu na wanachama wa muungano wa wanawake wa Lamu Women Alliance (LAWA) wamejitokeza kukashifu vikali mauaji ya kiholela dhidi ya wanawake yanayoendelezwa humu nchini karibu kila siku.

Maimamu na Maustadh, wakishirikiana na wanawake hao sasa wanahusisha mauaji hayo ya kinyama na ibada za kishetani.

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Viongozi wa Dini Pwani – Coast Interfaith Council of Clerics, Ustadh Mohamed Abdulkadir, alisema wakati umewadia kwa viongozi wa dini zote humu nchini kuja pamoja na kufanya maombi maalum ya kufurusha pepo wabaya wanaowaingia wanaume kwa wanawake ambao mwishowe huishia kuuana.

Wanawake wakifuatilia kikao kisiwani Lamu. Picha|Kalume Kazungu

“Yanayofanyika hapa nchini, hasa haya mauaji ya wanawake, ni ushetani mtupu. Ninashuku huenda hao wanawake kwa wanaume wanaoendeleza vitendo hivyo wamejiingiza katika ibada za kishetani. Ni nguvu hizo za giza ambazo zinawasukuma kutekeleza vitendo vya kihayawani kama kuuana, kukatanakatana viungo, kubakana na mengine mengi yasiyotajika,” akasema Bw Abdulkadir.

Imamu wa Msikiti wa Jamia Mjini Mokowe, Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Bwanamkuu alitaja kufeli kwa wazazi kimalezi kuwa miongoni mwa changizo za maovu yanayoshuhudiwa kila mara, ikiwemo hayo mauaji ya wanadada.

Bw Bwanamkuu alishikilia haja ya wazazi kuwakuza watoto wao katika njia ya kumuogopa Mungu, kuwa waaminifu na kuepuka hulka ya tamaa ili wasijipate pabaya.

Aliwalaumu wazazi ambao hawafuatilii kamwe mienendo ya watoto wao punde wanapobaleghe, iwe ni mabarobaro au mabanati.

“Utapata mzazi akimpa uhuru msichana au mvulana wake kupita kiasi. Watoto, hasa wanapojiunga na chuo kikuu basi hapo utampata mzazi akikosa kabisa kuwajibikia malezi. Lazima tufuate hiyo mienendo ya watoto wetu, hasa hawa wasichana kwa karibu zaidi. Tuwafunze kutosheka kwa wanachokipata ili wasijiingize kwenye nuksi za wanaume, kujichanganya na kisha kuishia kuuawa,” akasema Bw Bwanamkuu.

Naye Afisa Mtendaji wa Lamu Women Alliance (LAWA), Bi Raya Famau alilaumu waja kwa kuacha dini na tamaduni na badala yake kufuata mienendo ya kiulimwengu inayowapotosha.

Alitaja tabia za wanawake kwa wanaume kujiingiza katika masuala ya anasa, hasa ngono-biashara, ambapo hatua hiyo imeishia kuangamiza wengi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Lamu Women Alliance (LAWA) Raya Famau. Asema utovu wa maadili, kuacha dini, mila na tamaduni ni changizo za mauaji, ikiwemo mauaji ya wanawake kiholela nchini. Picha|Kalume Kazungu

Bi Famau aliwashukuru viongozi wa dini ya kiislamu Lamu kwa kuendeleza maombi maalum kila Ijumaa misikitini katika harakati za kukemea mauaji yaliyokithiri ya wanawake nchini.

“Ni wakati ambapo serikali yafaa kutangaza mauaji ya wanawake kuwa janga la kitaifa. Ila cha msingi ni watu wazingatie dini na tamaduni. Unapokuwa mtiifu wa dini, iwe ni Uislamu au Ukristo utajikataza mambo fulani. Pia tamaduni zetu hutuzuia na kutuelekeza kunakofaa,” akasema Bi Famau.

Ripoti ya kuhofisha iliyotolewa hivi majuzi ilionyesha kuwa wanawake nchini Kenya wanazidi kuteswa na kuuawa kikatili kila siku.

Vituo vya uokoaji nchini vilionyesha kwamba visa 4000 vya dhuluma dhidi ya wanawake huripotiwa kila mwezi.

Kwa upande mwingine, polisi wanasema wamerekodi visa 97 ndani ya miezi mitatu.

Takwimu hiyo inaonyesha wazi kwamba kila muda wa saa ishirini na nne, kisa cha mwanamke kuuawa huwa kinaripotiwa nchini Kenya.