‘Nimefaulu kuzima unyanyapaa kwa kuambia watu wazi wazi nina virusi vya Ukimwi’
DANIEL Muiyoro Kimani amekuwa akiishi na virusi vya Ukimwi kwa miaka 28 sasa.
Bw Kimani, 53, ambaye ni baba wa watoto watano, anasema amekuwa akikabiliana na unyanyapaa katika jamii kupitia kutangaza hali yake ya virusi paruwanja.
Anasema badala ya kusubiri kushuhudia watu wakimnyoshea vidole kisiri na kunong’onezana kwamba ‘muone jamaa yule ana Ukimwi,’ yeye huhakikisha umma tayari una taarifa za mapema kuhusu hali yake ya virusi vya Ukimwi, hivyo kuunyamazisha.
Bw Kimani alijipata akiugua Ukimwi mnamo 1996 kwa wakati huo akiwa umri wa miaka 24 pekee.
Alikuwa bado hajaoa na hana mtoto.
Baada ya kugundua kwamba anaishi na Ukimwi, Bw Kimani aliamua kujiunga na kundi moja la ushauri wa kijamii lililojumuisha sana watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi eneo la Mpeketoni, kaunti ya Lamu.
Ni kupitia utangamano na mtagusano kati ya washirika hao ambapo Bw Kimani alifaulu kujishindia mwenza wake wa maisha, Bi Pauline Njeri Mwangi ambaye pia ni mwaathiriwa wa virusi vya Ukimwi.
Baada ya kufuata ipasavyo ushauri wa kiafya, matibabu na kliniki kwa jumla, Bw Kimani na Bi Njeri, 44, walianza familia na kufikia sasa wana watoto watano ambao wote hawana virusi vya Ukimwi.
Kifungua mimba wao yuko na miaka 26 ilhali wa pili akiwa miaka 21.
Wa tatu ana miaka 14 ilhali wa nne akiwa miaka 11.
Kitinda mimba wao yuko na miaka minne.
Bw Kimani anasisitiza kwamba kujipata na virusi vya Ukimwi kamwe siyo mwisho wa maisha kwani waja bado wanaweza kuishi raha mustarehe.
“Cha msingi ni mtu kujikubali anapojipata katika hali ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi. Lazima pia watu wajikaze kufuata ushauri wa matibabu na kliniki. Mnapofanya hivyo basi mtajipata mkizaa watoto wasiokuwa na virusi licha ya nyinyi wenyewe kama wazazi kuwa na Ukimwi. Hilo naweza kulishuhudia kwa uhakika kwani limenitendekea kwangu binafsi,” akasema Bw Kimani.
Anashauri jamii kuwakubali waathiriwa wa virusi vya Ukimwi pasipo kuwabagua na kuwasimanga kwani hali hiyo imewasukuma wengi kuishi maisha ya siri bila kufichua hali zao.
Anataja kisa ambapo siku moja alihudhuria hafla fulani, ambapo wakati chakula kikisambazwa, mmoja wa akina dada waliokuwa wakisambaza sinia alimnong’onezea mwenzake kwamba asimpe sinia ya pilau Bw Kimani eti kwa sababu aliugua virusi vya Ukimwi.
“Karibu nilie mwanadada alipomnong’onezea mwenzake kwamba ‘usimpatie chakula huyo ana virusi vya Ukimwi.’ Watu wafahamu kwamba Ukimwi hausambazwi kupitia kutumia sahani moja za chakula. Virusi vitasambaa tu pale kutakapokuwa na mtagusano wa moja kwa moja kati ya damu ya mwaathiriwa na ile ya asiye mwathiriwa. Pia ngono husambaza ukimwi mara moja. Tusibague wenye ukimwi kwa misingi isiyofaa,” akasisitiza Bw Kimani.
Anawashauri wale wanaoishi bila virusi kuwa waangalifu na kuepuka kushiriki ngono kiholela bila kinga.
“Kama wewe ni mtoto ambaye ni chini ya miaka 18, basi kujiepusha kufanya mapenzi ndilo jambo la busara. Kwa wale watu wazima, tumia kinga ama uwe na mpenzi mmoja mnayeaminiana ili kujiweka salama,” akasema Bw Kimani.
Aidha anajutia jambo moja maishani, kwamba alitumia ujana wake vibaya kwa kushiriki ngono kiholela na warembo bila kinga, kunywa pombe kupita kiasi na kuvuta bangi, hali anayoitaja kuchangia hali yake ya sasa ya virusi vya Ukimwi.
“Nisingetumia ujana wangu vibaya, singekuwa ninaugua Ukimwi. Fedha nyingi nilizoiba dukani kwa mamangu na zile nilizopewa na wajomba na mashangazi zilipelekea mimi kuishi maisha ya anasa bila umakinifu hadi nikaambukizwa Ukimwi,” akasema Bw Kimani.
Aidha anasisitiza haja ya wenye ukimwi kuwafahamisha watu wa familia, ikiwemo mke, watoto, wazazi na wengineo badala ya kuishi kisiri.
“Mimi na mke wangu tunajuana hali zetu za Ukimwi. Watoto wetu pia wanafahamu kwamba tunaishi na virusi vya Ukimwi. Hao ndio utawapata wakituhimiza kunywa dawa, kutuletea na maji ili tutumie wakijua fika umuhimu wa tiba hiyo kwetu kama wazazi wao. Hilo limepunguza presha kwa familia,” akasema Bw Kimani.