NISHATI YA UPEPO: ERC yakubalia kampuni ya Ubelgiji kuanza kazi Lamu
NA KALUME KAZUNGU
TUME ya Kudhibiti Kawi nchini (ERC) hatimaye imepitisha ujenzi wa mradi wa nishati ya upepo katika eneo la Baharini, tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu.
Mradi huo unaokadiriwa kugharimu kima cha Sh21 bilioni uko chini ya ufadhili wa kampuni ya Ubelgiji ya Elicio kwa ushirikiano na Kenwind Holdings ya humu nchini.
Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 90 za umeme punde utakapokamilika.
Akizungumza na wanahabari mjini Lamu Jumanne, Afisa Msimamizi wa Mradi huo, Susan Nandwa, alisema ERC imepasisha na hata kutoa tarehe kamili ya kuanzishwa kwa mradi huo eneo la Baharini.
Kwa mujibu wa Bi Nandwa, awamu ya kwanzaya utekelezaji wa mradi huo itakuwa ni kuzalisha megawati 50 ambapo shughuli hiyo inanuiwa kuanza Januari, 2021.
Awamu ya pili itakuwa ni kuzalisha megawati 40 za umeme ambapo shughuli hiyo imepangwa kutekelezwa Januari, 2022.
Bi Nandwa aliipongeza ERC kwa kuupasisha mradi huo.
Tangu 2011, mradi huo wa upepo umekuwa ukipokea pingamizi chungu nzima, ikiwemo kampuni ya Kenwind Holdings kushtakiwa na ile ya Cordison International ambayo ilidai Kenwind ilipendelewa na Tume ya Ardhi nchini (NLC) na kupewa nafasi kuendeleza mradi huo katika eneo la Baharini ambalo si lake.
Kesi hiyo aidha ilifutiliwa mbali mnamo Mei mwaka huu.
“Nimefurahia hatua ya ERC ya kupasisha mradi wetu wa nishati ya upepo eneo la Baharini. Tayari tumekabidhiwa tarehe kamili ya kuanzisha shughuli za mradi. Awamu ya kwanza itatekelezwa Januari, 2021 na ya pili itekelezwe Januari, 2022,’ akasema Bi Nandwa.
Alisema lengo lao hasa ni kudumisha uhusiano mwema na wakazi wa eneo hilo la Baharini ili kuhakikisha mradi unafaidi zaidi jamii ya eneo husika.
Hatua ya kupasishwa kwa mradi huo ni afueni kwa zaidi ya wakulima 600 wanaomiliki ardhi za eneo linalonuiwa kujengwa kiwanda hicho, ambao kwa zaidi ya miaka minane sasa wamekuwa wakisubiri kupokea fidia ili kupisha ujenzi wa mradi huo.
Jumla ya ekari 3,206 za ardhi zimetengwa eneo la Baharini ili kufanikisha mradi huo.
“Tumepokea habari za kupasishwa kwa mradi na ERC kwa furaha kubwa. Sisi tumeukubali mradi na tuko tayari kupokea fidia ili kupisha mradi uendelee eneo letu,” akasema Mwenyekiti wa Wakulima wa Baharini, Bw Linus Gitahi.
Naye Bw Zacharia Ng’ang’a, aliutaja mradi huo kuwa wa natija tele kwa jamii ya eneo hilo.
Alisema mradi huo ukianza kutekeleza shughuli zake kijijini mwao utaleta ajira kwa vijana na pia kupanua Lamu kibiashara na kiviwanda.