Nitarekebisha mambo nikiwa Rais wa Kenya Matiang’i asema
ALIYEKUWA Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i ameahidi kurekebisha hali nchini kwa kuondoa changamoto zinazokumba sekta muhimu za elimu, afya na usalama miongoni mwa zingine akichaguliwa kuwa rais 2027.
Kulingana na mgombeaji huyo wa urais wa chama cha Jubilee, utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo na mpango wa afya kwa wote (UHC) unakumbwa na changamoto kwa sababu serikali ya Rais William Ruto “inaelekeza rasilimali nyingi katika shughuli zisizo muhimu.”
“Kwa mfano mnamo Januari kati ya asilimia 20 na asilimia 30 ya watoto hawatahudhuria shule kwa sababu wameanzisha utozaji karo katika shule za upili za kutwa na kuweka karo ya Sh53, 000 katika shule za mabweni. Ni wazazi wangapi watamudu gharama hiyo?” Dkt Matiang’i akauliza.
Alisema uwezo wa kifedha wa wazazi wengi umepungua kutokana na mzigo mkubwa wa ushuru waliowekewa na serikali.
“Tunahitaji kurekebisha hili kwa kuelekeza rasilimali za kutosha katika mpango wa elimu bila malipo,” Dkt Matiang’i akasema Jumatano Novemba 19, 2025 asubuhi kwenye mahojiano kwenye kipindi cha “Fixing The Nation” kwenye runinga ya NTV.
Mgombeaji huyo wa urais aliisuta serikali ya Rais Ruto kwa mwenendo wa kucheleweshwa kwa pesa za kufadhili masomo akisema hali kama hiyo haikushuhudiwa alipohudumu kama Waziri wa Elimu katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
“Utoaji wa pesa za masomo ulicheleweshwa tu nyakati za msimu wa kisiasa au wakati wa janga la Covid-19. Aidha, serikali haikupunguza mgao wa fedha hizo kiholela inavyofanyika sasa,” akaeleza Dkt Matiang’i.
Aliahidi kuziba mianya ya ufujaji wa pesa za umma katika sekta ya elimu kwa kurejelea mfumo wa kitaifa wa kubaini idadi ya wanafunzi shuleni (NEMIS).
Kuhusu utekelezaji wa mpango wa afya kwa wote (UHC), Dkt Matiang’i alisema japo serikali ya Kenya Kwanza inauendesha kupitia bima inayosimamiwa na mamlaka ya afya ya kijamii (SHA), bado kuna changamoto.
“Shida ni kwamba viongozi wa serikali wamefumbia macho changamoto zinazoisibu SHA. Wananchi wanalia kule mashinani ilhali maafisa wa serikali wanadai utekelezaji wa bima hiyo unaendeshwa vizuri,” Dkt Matiang’a akasema.
“Tutahakikisha kuwa mpango wa UHC unatekelezwa ipaswavya kwa kurekebisha bima ya sasa ya SHA kwani malengo yake ni mazuri,” akaongeza.
Waziri huyo wa zamani aliahidi kurekebisha changamoto zinazokumba sekta ya usalama nchini, haswa Idara ya Polisi.
“Maafisa wa polisi bado wanalalamikia ukosefu mahitaji ya kimsingi kama mafuta kiasi kwamba hawawezi kutekeleza majukumu yao ya kulinda usalama. Tunaweza kurekebisha hilo,” Dkt Matiang’i akaeleza.
Kwa mara nyingine Naibu huyo wa Kiongozi wa Jubilee alijitenga na visa vya mauaji ya kiholela viliyodaiwa kutekelezwa na polisi kati ya mwaka wa 2019 hadi 2021 alipohudumu kama Waziri wa Usalama.
Zaidi ya maiti ya 200 ya waliouwa ilitupwa katika Mto Yala, katika kaunti ya Siaya.
“Nimelijibu swali hili sasa mara ya saba na sitachoka kujibu. Miili ilipopatikana katika mto Yala, nilishauri kufanyike uchunguzi. Lakini polisi walikataa wakisema watu wa familia wangetambua miili hiyo hali ambayo ingesaidia katika uchunguzi kuhusu kiini cha mauaji yao,” Dkt Matiang’i akasema.
Alipendekeza kuwa kubuniwe kwa kamati maalum ya kuchunguza mauaji hayo “ili ukweli ubainike”.
“Niko tayari kujiwasilisha mbele ya kamati kama hiyo, ikiongozwa na jaji mwenye uzoefu mkubwa, kusema yale yote ninayofahamu kuhusu maovu hayo,” Dkt Matiang’I akaeleza.