OBARA: Kinaya cha mwaka vijana kumrai Raila awakomboe
Na VALENTINE OBARA
HAYAWI hayawi hatimaye huwa. Licha ya kilio kutoka kwa wananchi wengi hasa wenye mapato ya chini, mswada wa fedha hatimaye uliidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta ukiwa na ushuru mpya kwa Wakenya.
Dalili zilikuwa wazi kwa yeyote anayefahamu vyema siasa za nchi hii kwamba mswada huo ungepita kwa njia yoyote ile. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwani sauti ya mwananchi ilipuuzwa hata bungeni.
Kwanza ningependa kuchukua fursa hii kuwapongeza wabunge waliosimama kidete na wananchi wengi wanaolemewa kiuchumi kupinga sheria hiyo ya ushuru mpya.
Wakati wote ambapo kulikuwa na mdahalo mkali kuhusu mswada huo ambao sasa ni sheria, kuna baadhi ya watu ambao walimlaumu Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa kutoupinga kwa msingi wa muafaka wake na rais.
Kinachonisikitisha ni kuwa miongoni mwa waliokuwa wakimlalamikia Bw Odinga ni idadi kubwa ya vijana hasa katika mitandao ya kijamii.
Vijana wanafaa kufahamu kuwa huu ni wakati wao wa kuamua jinsi serikali inavyosimamiwa na ni aibu kubwa wanapomlalamikia mwanasiasa mkongwe bila kujitolea wenyewe kupigania haki wanayotaka.
Katika enzi hii, kizazi cha sasa kina uwezo bora zaidi wa kutetea haki za wananchi wote. Lakini hilo halitatendeka kama vijana wataendelea kujificha nyuma ya skrini za simu zao na tarakilishi wakipiga kelele mitandaoni bila kuchukua hatua yoyote mwafaka.
Vijana wengi wamekuwa wazembe. Hawataki kutoa jasho, na hili sio tu katika masuala ya kupigania uongozi bora bali pia kujiendeleza maisha yao wenyewe.
Tumekuwa kizazi cha kutafuta mtu wa kulaumu kila mara tunapokumbwa na changamoto yoyote maishani mwetu. Hatutaki kujikagua nafsi zetu wenyewe ili tutambue hila tulizo nazo na kujirekebisha.
Tofauti na ilivyokuwa zamani, tuna katiba ambayo imelinda haki zetu kwa njia inayotupatia mandhari bora ya kupigania haki za kijamii.
Vile vile, tumejaliwa teknolojia za kisasa ambazo tunaweza kutumia kujifahamisha mengi ya kutusaidia katika juhudi hizi na pia kueneza ujumbe huo kwa umati mkubwa zaidi kwa kasi.
Lakini tumeamua kwamba teknolojia ni ya burudani, na kwa wengine ni mfumo wa kufanya vitendo vya ulaghai kujipatia riziki huku wengine wakipata nafasi ya kumtusi Bw Odinga kupitia mitandao hiyo.
Kuna mataifa mengi ambako vijana wametumia mitandao ya kijamii kuleta mabadiliko wanapohisi kukandamizwa. Hata kama walisaidiwa na wanasiasa wakongwe, hawakukaa kitako wakilialia jinsi tufanyavyo.
Hakika, hata humu nchini kuna masuala kadhaa ambayo yametimizwa kufuatia kilio cha wananchi mitandaoni.
Hizi ni ushahidi tosha kwamba vijana wana uwezo wa kufanya serikali isikilize na itekeleze maoni yao kuhusu uendeshaji wa taifa.
Huu si uchochezi wa mapinduzi, bali ni uchochezi unaolenga kuhamasisha vijana wachukue nafasi yao katika masuala ya uongozi wa taifa. Wakome kutumia nguvu na maarifa zao isivyostahili huku wakisubiri ukombozi ambao hauonekani karibu upeoni mwa macho yetu.