Makala

OBARA: Muafaka usiwe siasa tu bali uinue maisha ya raia

December 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

USHIRIKIANO wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, unaazidi kusifiwa kutoka pande tofauti.

Sifa hizi zilizoenea kitaifa ambazo zinaendelea kuwaletea wawili hao fahari kubwa pamoja na tuzo za kipekee ni kwa sababu ya amani inayoshuhudiwa nchini, tofauti na ilivyokuwa katika awamu ya kwanza ya utawala wa Jubilee kulipokuwa na uhasama kati ya serikali na upinzani.

Kwa sasa, tukielezana ukweli, mwananchi wa kawaida hajafanikiwa kuvuna matunda ya ushirikiano huu ipasavyo kwani changamoto tele zingali zinamkumba kimaisha.

Tatizo kuu zaidi ni kwamba gharama za mahitaji ya kila siku kwa mwananchi zimepanda hasa kutokana na ongezeko la ushuru wa bidhaa muhimu, hali iliyosababishwa na jinsi serikali ilivyokopesha kiwango kikubwa kupita kiasi cha fedha kutoka kwa mataifa ya kigeni.

Ninachofahamu ni kuwa ingawa Rais Kenyatta na Bw Odinga hutuambia hadharani kuwa ushirikiano wao ni kwa malengo ya maendeleo na wala si kwa minajili ya siasa, hawa wawili ni wanasiasa na anayeamini kwamba hakuna siasa katika maelewano yao, anajipumbaza.

Matumaini yangu ni kuwa hata wanapoendeleza siasa zao kisiri, hawatasahau kuhusu masilahi ya raia wa kawaida.

Mwananchi katika taifa hili amekuwa akitegemea zaidi mchango wa upande wa upinzani wa kisiasa kutetea masilahi yake lakini sasa upinzani ulimezwa na unaimba wimbo mmoja na serikali.

Katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Jubilee, serikali iliamua kwa hiari yake kutokabiliana na changamoto kuu za kitaifa hasa ufisadi licha ya onyo kutoka kwa upinzani wakati huo.

Kutokana na hili, siamini kwamba upinzani ndio ulikuwa kikwazo kwa serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi jinsi baadhi ya viongozi wanavyotaka tuamini.

Ukweli ni kwamba serikali ilikuwa na majivuno, haikutaka ushauri wowote wa nje na ilijifanyia mambo ikiwa tu na lengo la kulinda mahitaji ambayo yangeiwezesha kurejea mamlakani kwa awamu ya pili ya uongozi.

Matokeo yake ni uozo wa kitaifa ambao ndio sasa inajaribu kusafisha, na viongozi wa upinzani wamekubali kutoa mchango wao.

Inaeleweka kwamba pengine tunahitajika kuwa na subira ili mwananchi wa kawaida aanze kuona matunda halisi ya muafaka uliopo kati ya viongozi hao wawili.

Hivyo basi, yale ambayo hivi sasa tunaambiwa ni matunda ya muafaka si matunda kwa kweli bali ni mbegu tu zilizozikwa mchangani.

Hakika, tumepanda mbegu za amani na maendeleo. Kumea na kunawiri kwa mbegu hizi kutategemea zaidi misingi itakayoekwa ili isiwe kwamba ifikapo uchaguzi wa 2022, tutarejelea kule tulipokuwa kabla Machi 9, 2018 kwa kurudia uhasama wa kisiasa tuliozoea.

Mwananchi wa kawaida ataridhika tu kama miradi na mipango inayoekewa misingi sasa kuboresha hali ya maisha itazidi kuendelezwa kwa muda wa kudumu hata baada ya Rais Kenyatta kuondoka mamlakani.

Bila hilo, muafaka utaishia kuwa tu siasa za peni mbili ambazo raia amezoea kutapeliwa nazo.