OBARA: Sonko akejeliwe ila haki yake apewe
Na VALENTINE OBARA
KATIKA siku za hivi majuzi, Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa mienendo inayoonekana kwenda kinyume na maadili ya uongozi.
Wakosoaji wake wamekuwa wakimtia makucha tangu sikukuu ya Madaraka Dei ambapo alimtolea majibu makali Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti hiyo, Bi Esther Passaris hadi kumfanya aondoke mkutanoni gavana akiendelea kumjibu.
Baada ya hapo, Bw Sonko alizidi kuwasha moto kwa kufichua rekodi za mawasiliano ya simu alizodai zilikuwa za kibinafsi kati yake na Bi Passaris, na vilevile stakabadhi alizodai zilihusu malipo yaliyotolewa na serikali ya kaunti kwa mwakilishi huyo wa wanawake.
Hakuna pingamizi kwamba mienendo hii ya Bw Sonko haistahili kwa kiongozi mwenye mamlaka kama yake hasa anayesimamia kaunti ya Nairobi iliyo jiji kuu la nchi na lenye umuhimu mkubwa kimataifa, lakini si haki kwetu kutumia hili pekee kama kigezo cha kuamua kama uongozi wake umefana au kufeli.
Kwanza, yale tunayoona kutoka kwa gavana huyo mtatanishi si jambo geni. Bw Sonko amekuwa na vituko tangu wakati alipokuwa mbunge.
Isitoshe, siasa za Kenya ni chafu tangu jadi. Si rahisi kupata mwanasiasa aliye mamlakani hivi sasa tunayeweza kusema ana mienendo inayofuata mahitaji ya kikatiba kuhusu maadili mema.
Kwa ni kupigana hadharani, wamo. Ufujaji wa pesa za umma, hawakosekani. Kwa matusi nako huwawezi!
Kama kweli tunataka kujadiliana kuhusu mafanikio au kutofanikiwa kwa uongozi wa Bw Sonko, itakuwa vyema kuweka kando hisia zetu za kibinafsi ndipo tuanze kuchanganua utawala wake.
Tutahitajika kulinganisha hali ilivyo Nairobi sasa na ilivyokuwa wakati wa usimamizi wa aliyekuwa gavana wa kwanza, Dkt Evans Kidero.
Ingawa Bw Sonko hajafanikiwa kutekeleza matarajio ya wakazi wa Nairobi kwa asilimia mia moja, mgala muue na haki yake mpe.
Kufikia sasa, kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo ilitekelezwa na serikali hii ya kaunti ya Nairobi kwa kipindi cha miaka miwili pekee, ambayo hatukuona hata ikiguswa wakati wa utawala uliotangulia wa kaunti.
Huenda ikawa maendeleo hayo kama vile ujenzi wa barabara mitaani, ukarabati wa mifereji ya kusambaza maji, uboreshaji wa hospitali za kaunti na uzoaji wa taka hayaenei kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kwa sababu ni miradi inayofanywa katika mitaa ya wenye mapato ya chini ambao walitelekezwa tangu jadi.
Hatuwezi kushinda tukisambaza picha za sehemu chache za barabara mbovu zilizo katikati ya jiji na jaa za taka zinazosubiri kuokotwa kisha tuseme utawala umefeli.
Sikatai kuwa Kaunti ya Nairobi inastahili hadhi bora zaidi kimataifa kuliko ilivyo sasa. Lakini hili litatimizwa tu iwapo tutakuwa waaminifu katika jinsi tunavyokashifu viongozi, la sivyo tutaishia kupata kiongozi mwenye nidhamu machoni mwa jamii ila hana uwezo wowote kuleta mabadiliko tunayotamani.