Makala

Oburu awasihi vijana wasitoroke ODM bali waiimarishe kuelekea 2027

Na CHARLES WASONGA October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI mpya wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM Oburu Oginga, amewataka viongozi vijana kusalia katika chama hicho ili kukipa nguvu kuelekea 2027 akiapa kuwaunga mkono kufikia ndoto zao.

Akiongea Jumanne usiku katika runinga moja inayopeperusha matango kwa lugha ya dholuo, Dkt Oburu alikariri kuwa hamna mipango ya kuwafurusha viongozi kama vile Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino “kwa sababu hawajafanya kosa lolote kwa kuwa na misimamo mikali”.

“Sifuna hawezi kutimuliwa kwa sababu hamna kosa alilofanya. Sifuna ako sawa na tumeongea naye kwa sababu nyakati fulani damu yake huwa moto kwani yeye ni kijana. Hata Babu Owino na wengine hawaendi popote,tunawahitaji kukipa chama chetu nguvu kuelekea uchaguzi mkuu ujao” Dkt Oginga.

Seneta huyo wa Siaya alisisitiza kuwa ajenda yake kuu wakati huu ni kupalilia umoja katika ODM baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wake Raila Odinga.

Ili kufanikisha ajenda hiyo, Dkt Oginga akaeleza kuwa chama kinahitaji mchango wa vijana ambao kulingana naye ni viongozi wa sasa wala sio kesho.

“Hii ndio maana namsihi kiongozi kama Babu Owino kwamba asitoroke. Asalie ndani ya ODM huku akiendeleza ndoto zake za kuwania ugavana wa Nairobi. Asubiri kushiriki mchujo pamoja na wengine watakaojitokeza na bila shaka ODM itamuunga mkono endapo atashinda,” akaeleza akiongeza kuwa ametuma watu fulani wamtafute Babu ili azungumze naye.

Mapema mwaka huu Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki alitangaza kuwa yu tayari kuwania ugavana wa Nairobi kama mgombeaji huru baada ya uongozi wa ODM kuonyesha dalili kuwa utamuunga mkono gavana wa sasa Johnson Sakaja.

“Ninajua kwamba hawatanipa tiketi ya kuwania kwa sababu tayari wamesema watamuunga Sakaja chini ya mwavuli wa serikali jumuishi. Lakini nimeapa kuwania ugavana wa Nairobi hata kama itabidi niwe mgombea huru,” Bw Owino akasema akijibu fununu kwamba Raila alimwahidi Sakaja uungwaji mkono.

Kuhusu kiongozi atakayekuwa msemaji wa jamii ya Waluo kisiasa, Dkt Oginga alisema kiongozi huyo anafaa kuwa mwenye umri mdogo.

“Mtu kama huyo hafai kuwa mzee kama mimi na Raila. Anafaa kuwa kijana atakayeibuka, mwenye nguvu na atakapata baraka kutoka kwa jamii yetu,” akaeleza huku akisema kuwa kiongozi kama huyo huwa hachaguliwi bali “huibuka kama uyoga.”

Dkt Oginga pia alisisitiza kuwa ODM itaendelea kuwa chama huru huku kikishirikiana na muungano wa Kenya Kwanza chini ya serikali jumuishi “hadi 2017”.

“Ushirikiano wetu na mrengo wa Rais Ruto imekita katika ajenda 10 zilizoko kwenye mkataba wa maelewano uliotiwa saini Machi mwaka huu. Tutasalia pamoja hadi 2017 huku tukikiimarisha chama chetu,” akaeleza.

Wakati huo huo, Seneta huyo ametoa wito kwa viongozi wa chama hicho wawasaidie vijana kujisajili kuwa wapiga kura ili washiriki katika uchaguzi mkuu ujao.