Makala

ODM@20: Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa ODM afichua jinsi Hayati Raila alivyomtafuta usiku Dandora

Na KEVIN CHERUIYOT November 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BARABARA zote wiki hii zinaelekea Kaunti ya Mombasa, ambako chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kitasherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

Hafla hiyo itawaleta pamoja viongozi wa chama na waanzilishi wake waliotoa mchango mkubwa katika kuzaliwa kwa chama hicho.

Miongoni mwa waanzilishi waliopokea mwaliko binafsi ni Bi Jane Wangui Muringi.

Ingawa si wengi wanaomfahamu katika uongozi wa ODM, Bi Muringi alikuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa chama hicho baada ya kusajiliwa rasmi kufuatia kura ya maamuzi ya mwaka 2005.

Akizungumza na Taifa Dijitali Novemba 12, 2025, Bi Muringi alifichua jinsi hayati Raila alivyosafiri usiku hadi Dandora kumtafuta, tukio ambalo alisema hatalisahau maishani mwake.

“Nilikuwa nyumbani jioni moja wakati Tony Gachoka aliniita na kuniambia yuko nje ya nyumba yangu. Nilimwambia ni usiku sana lakini alisisitiza nitoke. Nilipotoka, niliona gari kubwa, na kama msichana wa mitaani nilishtuka,” alisimulia.

Kwa mshangao wake, alielekezwa kwenye kiti cha nyuma cha gari hilo la kifahari  na humo alikutana ana kwa ana na ‘Baba’ mwenyewe, Raila Odinga.

“Huyo ni mtu ambaye nilikuwa namuona tu kwenye televisheni! Nilikaa naye nyuma ya gari, tukazunguka Nairobi, na nilitetemeka safari nzima,” alisema huku akicheka.

Wakili Mugambi Imanyara, aliyesajili ODM kwa mara ya kwanza kabla ya kuikabidhi kwa Raila na timu yake, alithibitisha kuwa Bi Muringi ndiye Katibu Mkuu wa kwanza wa ODM.

“Alikuwa Katibu Mkuu wetu wa kwanza kabla ya kumbadilisha na Tony Chege,” alisema.

Katika safari hiyo iliyowapeleka hadi Kibra na maeneo mengine ya jiji, Raila alimueleza kwa nini alimhitaji.

“Aliniambia, ‘una kile ninachohitaji zaidi, chama.’ Tulikuwa tumekisajili na Mugambi Imanyara. Mimi nilikuwa nataka mabadiliko, na Raila anaamini katika mabadiliko. Kwa hivyo nilimwambia ningempa chama,” alisema Bi Muringi.

Anasema hakuhitaji fidia yoyote wala nafasi maalum serikalini.
“Aliniuliza, ‘Taja bei yako.’ Nikamjibu, ‘Sihitaji pesa. Ninachotaka ni tufanye kazi pamoja kwa ajili ya mabadiliko.’”

Siku iliyofuata walikutana tena na kufanikisha makubaliano hayo, ambapo alijiuzulu rasmi kama Katibu Mkuu na kuteuliwa kuwa Katibu wa Mipango Maalum katika Baraza Kuu ya Kitaifa (NEC).

Wakati wa Serikali ya Muungano, Raila Odinga alimteua kuwa Mshauri wa Vijana katika Ofisi ya Waziri Mkuu, nafasi aliyosema ilitokana na uhusiano wao wa karibu wa kikazi.

“Baba ndiye aliniingiza serikalini. Nilimwona kama baba, mlezi na mwalimu. Miaka 20 baadaye, amedumisha ahadi zake. Alikuwa rafiki yangu na nguzo yangu,” alisema kwa hisia.

Mnamo  Septembac 30 alipokea barua kutoka kwa Raila Odinga mwenyewe, akimwalika rasmi kuhudhuria sherehe za ODM@20 mjini Mombasa.