• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
ODONGO: TSC imekubali kutumika kuvuruga demokrasia Kenya

ODONGO: TSC imekubali kutumika kuvuruga demokrasia Kenya

NA CECIL ODONGO

NI jambo la kusikitisha kuona uhusiano kati ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) na vyama vya kutetea maslahi ya walimu unaendelea kudorora, hali ambayo ni hatari kwa taaluma hii muhimu.

Kwa muda sasa, TSC imekuwa na uhusiano mbaya na chama cha KNUT kuhusu maswala mbalimbali kama vile nyongeza ya mishahara na mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa wanachama wao.

Si suala la kuficha kwamba tume hiyo kupitia Afisa Mkuu Nancy Macharia imekuwa ikitumia mbinu mbaya kugawanya KNUT na ili kuendeleza mtindo wa kufifisha nguvu za kutetea masuala yanayowaathiri walimu kikazi.

Tukio la wiki jana ambapo mazungumzo kuhusu makubaliano ya nyongeza ya mishahara maarufu kama CBA kati ya TSC na Kuppet yalisambaratika linaonyesha wazi jinsi tume hiyo haina nia ya kuwapa walimu fedha zaidi.

Kuppet imekuwa ikionekana kama chama kinachotumiwa na TSC kulemaza umaarufu wa Knut lakini hata wao sasa hawana lao kwa kuwa baadhi ya mapendekezo yao ya kuimarisha maisha ya wanachama wao sasa yanaendelea kukataliwa na tume hiyo.

Nikirejelea Knut, si siri kwamba TSC imekuwa ikiegemea upande moja kwenye mgogoro wa uongozi unaoendelea katika chama hicho.

Kwa mfano, tume hiyo, majuzi iliondoa jina la Katibu Mkuu Wilson Sossion kwenye sajili ya walimu sababu ikiwa pingamizi kuhusu utekelezaji wa mtaala mpya na pia kuteuliwa kwake kama mbunge maalum wa chama cha ODM.

Hata hivyo, hii ni kinaya kwa kuwa Mbunge wa Emuhaya, Omboko Milemba pia ni Mwenyekiti wa Kuppet na hatujaona akiagizwa aache wadhifa wake kwenye chama hicho ili aendelee kuhudumu kama mbunge.

Mkono wa TSC unaoenekana kuwa kwenye malumbano ya uongozi kati ya maafisa wa Knut ambao baadhi wamekuwa wakipigania kuondolewa kwa Bw Sossion katika wadhifa anaoshikilia.

Hili linazua maswali mazito kwa sababu hata Bw Sossion akiagana na Knut bado viongozi hawa wanaompinga watapigania maslahi yale yale yanayowahusu walimu, ambayo TSC imekuwa ikijikokota au kukataa kutekeleza.

Ni vyema kwa maafisa wa TSC kuwa wangwana na kukubali kufanya kazi kwa karibu na vyama hivi vya walimu ili kusitisha uhasama huu ambao unaendelea kuwaumiza walimu.

Haiwezekani kwamba TSC ndiyo huwa sawa kwa kila jambo huku ikiwatupia lawama Knut na Kuppet na kuwataka waonekane kama maadui wa serikali.

You can share this post!

MATHEKA: DPP hana nia ya kweli ya kupiga vita ufisadi nchini

TAHARIRI: Idara ya mahakama itengewe pesa zaidi

adminleo