Makala

ODONGO: Tuangazie utendakazi wa Raila, Ruto kuliko asili yao

December 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA CECIL ODONGO

WAKENYA hawafai kujiingiza kwenye siasa ambazo zinajikita katika kukosoa au kusifia uongozi wa familia kubwa zilizotawala siasa za taifa hili kwa muda mrefu dhidi ya wale waliokwea ngazi za uongozi kivyao.

Siasa hizi zimekuwa zikizingira familia za Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga, ambao wazazi wao walikuwa waanzilishi wa taifa hili kwa upande moja.

Kwa upande mwingine Naibu Rais William Ruto naye anatajwa kama mwanasiasa aliyejiinua kivyake na mtindo wake wa maisha unalingana na ule wa maisha ya raia wa kawaida.

Suala hili limekuwa likizua mjadala kati ya wafuasi wa viongozi hawa hasa ikizingatiwa kwamba Bw Odinga na Dkt Ruto huenda wakamenyana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wafuasi wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakidai kwamba familia hizo zilileta mageuzi makubwa ya kisiasa na uchumi nchini na utawala wao umesaidia Kenya kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa upande mwingine wafuasi wa Dkt Ruto wamelaumu utawala na uadui wa kisiasa kati ya familia ya Kenyatta na Bw Odinga kama uliochangia matatizo tele hasa umaskini ambao unaendelea kushuhudiwa nchini.

Hata hivyo, ni vyema kwa Wakenya kuangalia sifa ya kibinafsi ya kila kiongozi na sera zake kabla ya kumchagua badala ya kuangazia familia anakotoka au maisha yake ya utotoni.

Kwa mfano hapa nchini tangu mwanzo wa mfumo wa utawala wa ugatuzi kuna magavana ambao walijitosa uongozini kwa mara ya kwanza na rekodi yao ya maendeleo ni bora kuliko hata viongozi wengine ambao wameshikilia nyadhifa za uongozi kwa miaka kadhaa.

Kwenye uzi uo huo, kuna wabunge ambao wamehudumu kwa miaka kadhaa kutokana na rekodi yao ya kutumia vyema fedha za Hazina ya Maeneobunge (CDF) kuwafaa raia.

Badala ya raia kukabiliana mitandaoni kuhusu iwapo ni vyema kuchagua kiongozi kutoka familia zilizoshikilia nyadhifa za uongozi kwa muda mrefu na viongozi ambao wamejizolea umaarufu wenyewe, wanafaa kuanza kuangazia sera na uadilifu wa kila mwanasiasa.

Kwa mfano kuhusu Bw Odinga, raia wanafaa kuangazia rekodi yake miaka yote alipokuwa mbunge, waziri na hata waziri mkuu kabla ya kuamua iwapo anatosha kuwa rais au la.

Vivyo hivyo, wapigakura wanafaa kuangazia aliyoyafikia Dkt Ruto miaka ya nyuma akiwa mbunge wa Eldoret Kaskazini, waziri na sasa Naibu Rais kisha kuamua iwapo anatosha kuingia ikulu 2022 au bado hajaiva.

Cha kusikitisha hapa nchini hata hivyo ni wapigakura kuegemeza siasa zao katika mkondo wa kikabila na kupigia kiongozi wa jamii yao debe badala ya rekodi yake ya utendakazi na uwajibikaji.

Hii ndiyo maana baadhi ya wanasiasa wamehudumu kwa miaka mingi kwenye nyadhifa kadhaa kutokana na tabia yao ya kutowajibika baada ya kufahamu kwamba watarejea kwa wapigakura na mabunda ya noti kisha wachaguliwe tena.