Makala

Omtatah naye apinga sheria tata zilizotiwa saini na Rais Ruto

Na CHARLES WASONGA October 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SENETA wa Busia Okiya Omtatah amejiunga na orodha ya wale wanaoelekea kortini kupinga utekelezaji wa baadhi ya sheria zilizotiwa saini juzi na Rais William Ruto akisema zinakiuka Katiba.

Kwenye taarifa aliyochapisha Alhamisi katika akaunti yake ya mtandao wa X, Bw Omtatah alieleza kuwa  analenga kupinga sheria tatu miongoni mwa nane iliyotiwa saini Oktoba 15, 2025 ambazo pia alisema inaingilia uhuru wa Wakenya kujieleza.

“Kwanza ni Sheria ya  Marekebisho kuhusu Matumizi Mabaya ya Kampyuta inayohujumu uhuru wa Wakenya kujieleza na kupata habari. Inatisha kugeuza Kenya kuwa nchi hatari ambako mitandao ya kijamii inaweza kuzimwa kiholela. Nitawasilisha kesi kortini kupinga sehemu za sheria hii zinazokiuka katiba,” Bw Omtatah akasema.

Seneta huyo wa Busia pia anapinga Sheria ya Ubinafsishaji wa 2025, akisema nafasi ya kuuzwa kwa ardhi ya serikali na mali bila kuhusishwa kwa Seneti “ni kinyume na Kipengele cha 68 cha Katiba.”

“Ardhi ya umma ni muhimu zaidi, haiwezi kubinafsishwa,” akaeleza.

Vile vile, Bw Omtatah anapinga utekelezaji wa Sheria  (ya Marekebisho) ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi ya 2024, ambayo anasema inadhibiti mamlaka ya tume hiyo kwa kuiwekea makataa inaposhughulikia visa vya ukiukaji wa haki.

“Shughuli za usakaji wa haki kuhusu umiliki wa ardhi haiwezi kuharakishwa au kudhibitiwa

kupitia makataa yasiyo na maana, “ akaongeza.

Bw Omtatah ametangaza hatua hiyo siku moja baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi kusitisha kwa muda utekelezaji wa Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mitandaoni ya 2025.

Hii ni kufuatia kesi iliyowasilishwa na mwimbaji wa nyimbo za Injili na mwanasiasa Reuben Kagame na Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC).

Kulingana na Bw Kagame, kuna hatari kuwa sheria hiyo itatumiwa vibaya na serikali kuhujumu uhuru wa kujieleza, demokrasia na utawala bora.

Jaji Mugambi alisimamisha utekelezaji wa sheria hiyo hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.

Alhamisi, Seneta Omtatah aliwataka Wakenya kusimama ange kutetea utawala wa sheria.

“Sote tusimame kutetea Katiba na sheria husika. Sharti Kenya iongozwe kwa uzingativu wa Katiba, sio haja finyu za mtu mmoja au watu fulani wachache,” akaeleza.

Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) pia kimesema kijiunga na watu na makundi ambayo yameelekea kortini kupinga sheria hiyo na ile ya ubinafshaji mashirika ya umma.