Makala

ONYANGO: Kukwama kwa ‘Okoa Abiria’ kwazua maswali

October 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI ilizindua kwa mbwembwe mabasi 27 ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) mnamo Machi 2018 kwa lengo la kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano wa magari jijini.

Mabasi hayo yalizinduliwa mara baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na washikadau mbalimbali na kuwataka kuhakikisha kuwa wanashughulikia tatizo la msongamano wa magari jijini kwa haraka.

Mabasi hayo ya NYS yalihudumu katika barabara za kuelekea katika mitaa ya Embakasi, Githurai, Mwiki, Dandora, Kariobangi, Kibera, Kawangware, Kangemi na Kayole.

Mara baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo unaojulikana kama ‘Okoa Abiria’, wakazi wa Nairobi walihisi kupata afueni kwani abiria walitozwa nauli ya Sh20 tu bila kujali umbali.

Nauli hiyo ya chini iliwakera wamiliki wa magari ya usafiri wa umma ambao walidai kuwa ilikuwa pigo kwa biashara zao.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NYS wakati huo Richard Ndubai, ambaye sasa anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika sakata ya wizi wa fedha katika taasisi hiyo, alieleza Wakenya kuwa mabasi hayo yalilenga kutatua tatizo la msongamano wa magari ambalo limekuwa likizonga jiji la Nairobi kwa zaidi ya miongo miwili.

Kadhalika, Bw Ndubai aliambia Wakenya kwamba taasisi hiyo ingeongeza magari mengine 50 zaidi ndani ya kipindi cha miezi miwili ili kuwarahisishia wakazi wa Nairobi usafiri.

Ndubai alinaswa miezi miwili baadaye kabla ya kuongeza magari hayo namna alivyoahidi.

Mwaka mmoja baadaye, ripoti ya Mkaguzi Mkuu iliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya magari hayo yamekwama.

Mkaguzi wa Hesabu, katika ripoti yake alisema ni magari tisa tu yaliyokuwa yakihudumu kufikia Julai mwaka huu.

Kulingana na ripoti hiyo, serikali haijakuwa ikitengea hela mabasi hayo. Hali hiyo imeyasababisha mabasi hayo kukosa kukarabatiwa.

Ripoti hiyo ilimalizia kwa kusema kuwa “mradi huo wa Okoa Abiria ulikuwa unaelekea kusambaratika”.

Mnamo Aprili mwaka jana serikali iliidhinisha Sh500 millioni zitumiwe na NYS kununua mabasi zaidi.

Magari mengi ya usafiri wa umma jijini Nairobi yanamilikiwa na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Kukwama kwa mabasi ya NYS kunazua maswali tele.

Je, kuna uwezekano kwamba wanasiasa hao wanaomiliki, ndio wamekuwa wakihujumu mradi wa Okoa Abiria wa NYS?

Je, kuna mikono ya wanasiasa katika kukwama kwa mabasi hayo ambayo ni afueni kwa wakazi wa mitaa ambayo wengi wa wakazi ni wenye mapato ya chini?

Je, serikali inalenga kuachana na mradi huo baada ya kubaini kwamba haujafanya lolote kupunguza msongamano wa magari jijini?

Ikiwa kuna mkono wa watu fiche, Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) haina budi kufanya uchunguzi kuwanasa wahusika.