ONYANGO: Nia ya kufadhili vyama hivi vya kisiasa haifai
Na LEONARD ONYANGO
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkali kuhusu ugavi wa fedha za ufadhili wa vyama vya kisiasa kutoka kwa serikali; huku baadhi ya wanasiasa wakishinikiza sheria ifanyiwe mabadiliko ili vyama vidogo pia viweze kunufaika na mgao huo.
Mjadala huo ulishika kasi baada ya vyama vya Wiper chini ya kinara wake Bw Kalonzo Musyoka, Amani National alliance (ANC) inayoongozwa na Musalia Mudavadi na Ford Kenya ya Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kudai kuchezewa shere na chama cha ODM ambacho Raila Odinga ndiye kinara, kuhusiana na ugavi wa mamilioni ya fedha kutoka kwa Hazina Kuu ya Kitaifa.
Kulingana na sheria, vyama vya kisiasa vinafaa kupokea asilimia 0.3 ya mapato ya serikali kwa lengo la kuendeleza demokrasia.
Ili kunufaika na fedha hizo chama cha kisiasa ni sharti kiwe kimepata asilimia 3 ya kura za urais katika uchaguzi uliopita.
Asilimia 80 ya mgawo huo wa fedha inazingatia chama kilichopata kura nyingi, asilimia 15 hutolewa kwa kuzingatia idadi ya walemavu, wanawake na vijana waliopewa na chama husika.
Kwa kufuata kanuni hiyo ni vyama viwili pekee, Jubilee na ODM vinafaa kunufaika na fedha hizo kwani ndivyo vilifanikiwa kupata zaidi ya asilimia 3 ya kura katika uchaguzi uliopita.
Lakini vyama vya ANC, Wiper na Ford Kenya vinafaa kupewa mgawo na ODM kwa sababu viliunga mkono mwaniaji wake wa urais Bw Odinga katika uchaguzi uliopita.
Kulingana na takwimu zilizoko katika tovuti ya Msajiri wa Vyama vya Kisiasa zinaonyesha kuwa chama cha Jubilee Sh240 milioni na ODM Sh112 milioni kutoka kwa Hazina Kuu ya Kitaifa katika mwaka wa matumizi wa fedha uliokamilika Juni 30, mwaka huu.
Wanasiasa, haswa kutoka vyama vya ANC, Ford Kenya na Wiper sasa wanataka sheria ibadilishwe ili kuhakikisha kuwa vyama vidogo vinapata mgawo wa fedha kutoka kwa serikali.
Pendekezo hilo halifai na linalenga kuwanufaisha watu wachache wanasiasa.
Takwimu za Msajiri wa Vyama vya Kisiasa zinaonyesha kuwa humu nchini kuna vyama 78 vya kisiasa ambavyo vimesajiliwa.
Majina ya baadhi ya vyama; kama vile Grand Dream Development ambacho nembo yake ni gunia; Alternative Leadership Party of Kenya chenye nembo ya mshumaa, havijulikani hata miongoni mwa Wakenya.
Pendekezo la kutaka vyama vidogo vipewe ufadhili wa serikali ni kumtwika mlipa ushuru mzigo usio kuwa wa lazima. Hii ni kwa sababu vyama vya kisiasa humu nchini ni mali ya watu binafsi au kabila na havina manufaa kwa wananchi.
Vingi ya vyama hivi havina ofisi au ajenda yoyote ya maendeleo.
Kuna chama ambacho kimewahi kufanya uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi za mashinani isipokuwa ODM ambacho kilijaribu lakini shughuli hiyo ikagubikwa na mizozo si haba.