• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 3:16 PM
ONYANGO: Uhuru akifaulisha Ajenda 4 Kuu atakumbukwa zaidi

ONYANGO: Uhuru akifaulisha Ajenda 4 Kuu atakumbukwa zaidi

Rais Uhuru Kenyatta. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

BARAZA la Mawaziri sasa liko tayari kuanza kuwatumikia Wakenya baada ya mawaziri wengine tisa kuapishwa Ijumaa.

Mawaziri hao walioapishwa katika Ikulu ya Nairobi, walitakiwa kuhakikisha kuwa wanasaidia serikali kutimiza ahadi yake ya kufanikisha Ajenda Nne Kuu ambazo ni kuwapa Wakenya chakula cha kutosha, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, uboreshaji wa viwanda na kutoa huduma za matibabu ya gharama nafuu kwa kila Mkenya.

Rais Uhuru Kenyatta anaamini kuwa endapo ajenda hizo nne zitatekelezwa kikamilifu basi jina lake litaingia katika vitabu vya marais walioboresha maisha ya Wakenya na kustawisha uchumi wa nchi.

Inawezekana kutekeleza ajenda hizo kuu nne ikiwa serikali itazivalia njuga na kukoma kuingiza siasa katika miradi ya maendeleo.

Katika muhula wa kwanza Rais Kenyatta alinukuliwa mara kadhaa akiambia wakazi kuwa hawakumpigia kura.

Siasa za uchaguzi uliopita tayari zimeisha na sasa ni jukumu la viongozi waliochaguliwa kuwatumikia Wakenya bila kujali itikadi za vyama au kabila.

Kadhalika, mawaziri waliochaguliwa ni sharti waachane na itikadi ambayo imekuwepo kwa muda mrefu, kwa mfano, waziri wa Utalii anazuru na kuanzisha miradi katika maeneo ya Pwani au Mlima Kenya kwa sababu ndiyo hupokea idadi kubwa ya watalii.

 

Utalii maeneo kame

Maeneo ya Nyanza, Kaskazini Mashariki au Mashariki pia yanaweza kuwa vivutio vya watalii iwapo serikali itaweka mikakati ya kutosha.
Mara kadhaa tumeona mawaziri wa Kilimo wakizuru maeneo ya Bonde la Ufa na Kati kugawa mbegu na pembejeo nyinginezo.

Je, ni nani aliyesema kuwa maeneo ya Turkana, Kaskazini Mashariki, Ukambani na hata Nyanza hayawezi kutumiwa kuzalisha chakula?

Tatizo la ukosefu wa chakula cha kutosha linalokumba nchi hii linasababishwa na uzembe wa serikali kuendelea kutegemea maeneo machache kulisha nchi nzima licha ya idadi ya watu kuongezeka kila mwaka.

Mashamba makubwa katika maeneo ya Turkana, Kaskazini Mashariki na hata Ukambani hayalimwi au kufanyiwa shughuli yoyote ya kiuchumi kutokana na ukame.

Maeneo hayo yanaweza kutumika kulisha Wakenya ikiwa tutakumbatia mbinu za kisasa za kilimo kisichotegemea mvua.

Kadhalika, tumeona mawaziri wa Samaki na uvuvi wakitumia wakati wao mwingi kuzuru maeneo ya Ziwa Victoria na Bahari ya Hindi na kusahamu maeneo mengineyo yasiyokuwa na maziwa au bahari.

Samaki wanaweza kukuzwa kote almradi tutumie mbinu za kisasa.

You can share this post!

OBARA: Tusidanganyane, Kenya haitapata mageuzi punde

Sanchez hatarini kutemwa kwa kumezea mwanachuo

adminleo