Fahamu makosa ya kingono na adhabu za kila moja
Sheria ya Makosa ya Kingono Kenya ilileta mageuzi makubwa katika jinsi Kenya inavyokabiliana na makosa ya kingono.
Kabla ya sheria hii kutungwa, baadhi ya makosa haya hayakuwa yamefafanuliwa kikamilifu, na wale waliokuwa wakiyatekeleza mara nyingine walikwepa adhabu au walipata adhabu ndogo isiyolingana na uzito wa uhalifu.
Leo hii, sheria hii imesimama imara kama silaha dhidi ya unyanyasaji wa kingono kwa kuweka adhabu kali na zisizopingika kwa watakaopatikana na hatia. Makala haya yanachambua kwa kina adhabu kuu kwa makosa mbalimbali ya kingono nchini Kenya.
Ubakaji
Mtu yeyote anayepenya sehemu za siri za mtu mwingine kwa makusudi bila idhini, na kutumia nguvu, vitisho, au hila, anafanya kosa la ubakaji.
Adhabu ya ubakaji ni kifungo cha miaka 10 jela au zaidi, na kinaweza kuongezwa hadi kifungo cha maisha kulingana na hali ya kosa.
Sheria hii pia inatambua kuwa wanaume wanaweza kubakwa na wanawake au wanaume wengine – jambo ambalo halikuwa wazi katika sheria za zamani.
Jaribio la Kubaka
Kujaribu kumbaka mtu bila kufanikisha tendo hilo ni kosa linaloadhibiwa kwa ukali pia.Adhabu ya kosa hili ni kifungo cha miaka 5 au zaidi, na inaweza kufikia kifungo cha maisha.
Shambulio la Kingono
Hili ni kosa linalohusisha kupenya sehemu za siri za mtu mwingine kwa kutumia kiungo chochote cha mwili (isipokuwa sehemu za siri) au kifaa kingine chochote bila idhini yake. Anayetenda kosa hili anaweza kufungwa jela miaka miaka 10 au zaidi, hadi kifungo cha maisha.
Kupenya sehemu za siri kwa madhumuni ya kitabibu au usafi kwa idhini ya mtu hakuchukuliwi kama kosa.
Unajisi
Ulawiti ni tendo la ngono na mtoto yeyote mwenye umri chini ya miaka 18. Hata kama mtoto alikubali, tendo hilo ni kosa kubwa. Adhabu huwa ni kifungo cha maisha iwapo mtoto ana umri wa chini ya miaka 11, miaka 20 au zaidi jela iwapo mtoto ana umri wa kati ya miaka 12 na 15na miaka 15 au zaidi iwapo mtoto ana umri wa kati ya miaka 16 na 18.
Watoto hawawezi kutoa idhini ya kushiriki ngono kwa mujibu wa sheria na kukubali kwao si kinga kwa mtuhumiwa.
Mtuhumiwa anaweza kujitetea kwa kudai kuwa alidanganywa na mtoto kuamini ana umri wa zaidi ya miaka 18 au alifanya juhudi za kweli kujua umri wa mtoto.
Lakini utetezi huu haukubaliki iwapo mtuhumiwa ni ndugu wa damu wa mtoto.
Jaribio la kunajisi
Kujaribu kufanya ngono na mtoto bila kufanikisha tendo hilo huwa ni ni kosa na adhabu ni kufungwa jela miaka 10 au zaidi.
Mtuhumiwa anaweza kutumia utetezi sawa na wa unajisi, ila lazima aonyeshe alichukua hatua za busara kujua umri wa mtoto.
Ubakaji wa Kundi
Pale ambapo watu wawili au zaidi wanamshambulia mtu kingono kwa pamoja, kosa hilo linachukuliwa kwa uzito wa juu na adhabu yake ni kifungo cha miaka 15
Sheria hii pia imeweka adhabu kwa watu walio katika mamlaka au nafasi za kuaminika walimu, waajiri, viongozi wa dini wanaowatendea wengine makosa ya kingono. Makampuni yanayojihusisha na uhalifu kama ulanguzi wa wanawake, ponografia ya watoto, au kuwezesha unyanyasaji kingono.
Adhabu ni kutozwa faini kubwa, kufungwa kwa kampuni, na kufunguliwa mashtaka ya jinai kwa viongozi wake.