Pambo

Je, ni lazima mpenzi wako awe rafiki yako wa karibu?

Na WINNIE ONYANDO November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA ndoa au mahusiano yoyote ya kimapenzi, swali ambalo limekuwa likizua mjadala ni iwapo mpenzi wako anapaswa pia kuwa rafiki yako wa karibu au la.

Wapo wanaoamini kwamba penzi lolote lazima liwe na mizizi ya urafiki imara, huku wengine wakisema kuwa urafiki wa karibu si lazima. Lakini ukweli uko wapi?

Mshauri wa masuala ya ndoa, Stephen Kombo, anasema kwamba msingi mzuri wa uhusiano mara nyingi hutokana na urafiki, lakini hilo halimaanishi kuwa bila urafiki wa karibu hamuwezi kupendana.

“Watu wengi wanachanganya urafiki na upendo,” anasema.

“Urafiki unajenga mazingira ya usalama, uaminifu na kuelewana, lakini mapenzi yana nguvu yake ya kipekee hata kama hamkuwa marafiki wa muda mrefu.”

Kando na hayo, Stephen anaeleza kwamba kuwa na mpenzi ambaye pia ni rafiki wako wa karibu kuna faida nyingi.

Kwanza, inakuwa rahisi kuwasiliana bila hofu.

Mnaweza kushiriki ndoto, hofu, mafanikio na hata udhaifu wenu bila aibu.

Pili, migogoro inapojitokeza, mnayatatua kwa njia ya ustaarabu zaidi kwa sababu tayari mnajua namna ya kuzungumza kama marafiki.

“Uhusiano unaoanzia kwenye urafiki huwa na ustahimilivu mkubwa wakati wa changamoto,” anasisitiza.

Hata hivyo, mshauri huyo anatahadharisha kwamba si lazima kila mtu apate mapenzi kutoka kwa rafiki wa karibu.

Wapo wanandoa wengi walioingia kwenye mahusiano miezi michache baada ya kukutana, lakini walijenga mapenzi kwa kuheshimiana, kuelewana na kujifunza kile anachokipenda mwenzake.

“Kuna watu ambao urafiki wa karibu unaweza hata ukapunguza mvuto wa kimapenzi,” Stephen anaongeza. “Wengine wanapenda mipaka fulani katika maisha yao; wanataka mpenzi awe mpenzi, na rafiki awe rafiki.”

Kwa upande mwingine, kuwa na mpenzi ambaye sio rafiki wa karibu kunaweza kuleta changamoto.

Migogoro inaweza kuchukua muda mrefu kutatuliwa kwa sababu hakuna ule urafiki.

Stephen anasema hili linaweza kutatuliwa tu ikiwa wahusika wako tayari kujenga uhusiano wao kwa msingi wa urafiki.

Hata hivyo, Stephen anasema, “Sio lazima muwe marafiki ila la msingi ni nyinyi wawili kuamua kujenga uhusiano wenu kwa msingi wa urafiki.”

Katika safari ya mapenzi, urafiki ni kama upepo mzuri unaowasukuma kitaratibu na kuwawezesha kusonga mbele hata kukiwa na mawimbi.