Pambo

Leta mijadala katika masomo ya dijitali kwani hufaidi mwanao

Na BENSON MATHEKA April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUTOKANA na ongezeko la vifaa vya kielektroniki, watoto sasa wanatazama vitabu kwenye vifaa bebe.

Ni rahisi kuelewa mvuto wa vifaa hivi kwani hadithi zinachanganywa na picha za kupendeza pamoja na muziki wa kuwavutia watoto. Lakini je, mbinu hizi za kisasa za kusimulia hadithi zinaboresha ufunzaji wa watoto?

Kulingana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Vanderbilt, sehemu muhimu zaidi ya hadithi si jinsi mtoto anavyoiona, bali jinsi anavyoipitia na kuielewa. Kwa kusoma vitabu ana kwa ana na mtoto wako, mzazi hupata nafasi ya kuchambua hadithi na wahusika waliomo.

Aina hii ya kusoma inaitwa Usomaji wa Mazungumzo. Inawashirikisha watoto wadogo katika mchakato wa kusoma na hufaa watoto wa rika zote. Usomaji huu huwasaidia watoto wadogo kuwa wanafunzi wepesi kuelewa.

Kupitia maswali na mitazamo mbalimbali inayoibuka anaposhirikiana nsa mzazi kusoma, watoto wana uwezo mkubwa wa kufikiria kuhusu wanachokiona, kuunda uhusiano, kukuza ujuzi wa msamiati mpya, na kupata uzoefu wa hadithi.

Hata hivyo, aina hii ya ushirikishaji huwa nadra zaidi watoto wanapotazama hadithi kwenye vifaabebe.Katika utafiti uliohusisha wazazi 81 na watoto wao wa miaka mitatu, watafiti waliwapa watoto hao video za DVD zenye hadithi watazame kwa wiki nne.

Watoto walifanya mitihani miwili – kabla na baada ya majaribio, kuhusu msamiati na uelewa wa hadithi hizo. Katika matokeo ya utafiti, wazazi waliojadili hadithi hizo za DVD na watoto wao waliwafanya kupata alama za juu zaidi kwenye mtihani wa baada ya majaribio, kuliko watoto wa wazazi waliotazama tu video hizo bila kutoa maoni au kuuliza maswali.

Kwa kuwa hadithi za kielektroniki sasa zimekuwa sehemu ya elimu na maisha kwa jumla, kuna mambo ambayo wazazi wanaweza kufanya ili mbinu hii iwe ya maana zaidi na yenye manufaa kwa watoto wao — wachanganye Usomaji wa Mazungumzo na Masomo Dijitali.