Pambo

Mwaka mpya: Nafasi ya wanandoa kujijenga upya, sio kulaumiana

Na WINNIE ONYANDO January 11th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WANANDOA wengi huingia mwaka mpya wakiwa na orodha ya malengo ikijumuisha kujenga nyumba, kununua gari, kuanzisha biashara au kupata mtoto.

Hata hivyo, kuna jambo muhimu linalosahaulika mara nyingi: kujijenga kama mtu binafsi iwe kitabia au hata kielimu.

Wanandoa hujishughulisha na mambo mengi ikijumuisha kulea watoto na majukumu ya kila siku jambo linalowafanya wajisahau kabisa.

Mwaka mpya unapaswa kuwa nafasi ya wanandoa kujiangalia ndani, kutambua mapungufu yao na kujifunza namna bora ya kuishi pamoja.

Badala ya kuanza Januari kwa lawama na kumbukumbu za maumivu ya mwaka uliopita, ni vyema kuanza kwa kujitathmini na kuangazia namna ya kujiboresha na kufanya mahusiano kuwa bora zaidi.

Mtaalamu na mshauri wa masuala ya ndoa, Bw Vincent Ombok anasema changamoto nyingi katika ndoa hazichangiwi na ukosefu wa mapenzi bali ni kutokana na kutochukua muda kujijenga kama mtu binafsi.

“Unapokataa kukua, unamzuia hata mwenzako kukua. Ndoa ni safari ya watu wawili wanaojifunza kila siku,” anasema.

Kujijenga kibinafsi kunajumuisha kujifunza kudhibiti hasira, kuwasiliana kwa heshima, kusikiliza bila kukatiza au hata kukubali makosa na kuomba msamaha.

Kwa wengine, ni kujifunza kutibu majeraha ya zamani yaliyoletwa kwenye ndoa bila kujua.

Bw Ombok anashauri wanandoa waingie mwaka mpya kwa mazungumzo ya dhati.

“Kaa chini muulize mwenzako ni nini kilikuchukiza mwaka huu? Ni nini ningefanya tofauti? Ni wapi tunahitaji msaada?”

Maswali haya sio rahisi, lakini ni muhimu.

Aidha, kujijenga kunaweza kujumuisha kutafuta ushauri wa kitaalamu, kusoma vitabu vya ndoa, kushiriki semina au hata kuweka muda wa ubora wa kuwa pamoja bila simu wala vurugu za nje.

“Kumbukeni kuwa hatua ndogo ndogo huleta mabadiliko makubwa,” anasema Bw Ombok.

Mwaka mpya pia ni wakati wa kujifunza kujipenda.

Mtu anayejithamini, anayejijali kiafya, kiakili na kihisia, huleta amani zaidi kwenye ndoa.

Anasema kuwa huwezi kumpa mwenzako kile ambacho wewe mwenyewe huna.

“Utampendaje mwenzako usipojipenda wewe mwenyewe. Ikiwa hata huwezi kujinunulia nguo mpya, itamnunuliaje mwenzako? Hivyo basi, anza na wewe, jipambe na ujithamini.”

Bw Ombok anawanahimiza wanandoa wasitafute ukamilifu bali maendeleo mwaka huu mpya.

“Mwaka huu usiwe wa kulaumiana, bali wa kujenga, kuponya na kukua pamoja, hatua kwa hatua, kwa upendo na kwa uvumilivu,” anasema Bw Ombok.