Mwanamke pia ana uhuru wa kumtongoza mwanamume
WANANDOA wanapaswa kuwa wazi na kuzungumza bila kuficha chochote kuhusu suala la kushiriki mapenzi katika ndoa yao.
Ni muhimu kutambua kuwa ndoa haihusu tu kulea watoto au kushiriki majukumu ya familia, bali pia ni kufurahia na kudumisha mapenzi.
Hii inamaanisha kuwa pale unapomtamani mwenzako, hufai kuwa na aibu kumwonyesha au kumwambia hisia zako.
Wapo wanawake wengi ambao, kutokana na mila au imani walizolelewa nazo, wanaamini kuwa ni wajibu wa mwanaume kuanzisha tendo la ndoa.
Lakini ukweli ni kwamba, hata mwanamke ana jukumu na nafasi ya kuonyesha upendo wake kwa kumtongoza mume wake.
Mwanamke anaweza kuchukua hatua na kumshawishi mumewe kwa njia rahisi na ya kuvutia.
Zipo njia tofauti za kumuashiria mume wako kwamba ungependa kushiriki unyumba.
Mtongoze mchana
Usiwe yule mwanamke ambaye anajipenda tu na anataka aambiwe au afanyiwe kila mara. La! Kama mwanamke, mpe mume wako maneno matamu na ya kuvutia wakati wa mchana kwani ni njia nzuri ya kuamsha hisia za kimapenzi. Kwa mfano, unaweza kumtumia ujumbe mfupi wa kumkumbusha jinsi anavyokufanya uhisi anakupenda, au kumwelezea jinsi unavyotamani kuwa karibu naye.
Maneno kama haya huongeza msisimko na humfanya ahisi kuwa anathaminiwa. Wakati huu, haufai kumuelezea moja kwa moja, ila tumia maneno ambayo yatamuonyesha kuwa unamtamani.
Mavazi ya kuvutia hisia
Ikiwa mume wako hufika nyumbani usiku watoto wakiwa wamelala, tumia nafasi hiyo kumpa mapokezi ya kipekee. Valia mavazi yanayoonyesha sehemu zako za mwili kama vile mapaja na yanayokuvutia, pamoja na manukato unayojua anayapenda.
Kwa mfano, ikiwa una gauni zuri, jipambe kidogo na hakikisha unanukia vizuri. Acha mume wako avutiwe na kile anachokiona mbele yake – mapokezi ya kipekee huweza kumchemsha kihisia na kuongeza hamu ya kushiriki mapenzi nawe.
Vitendo vya kuonyesha mapenzi nyumbani
Mapenzi sio lazima yaonyeshwe chumbani pekee. Unapokuwa na mume wako nyumbani, ongeza ishara za kimahaba kama kumshika mkono, kumpa busu la ghafla, au kumkumbatia. Vitendo hivi humfanya ajihisi kuwa karibu nawe na hujenga msingi mzuri wa kushiriki tendo la ndoa. Kwa mfano, unaweza kumfuata jikoni au sebuleni, kumkumbatia kwa muda mfupi na kumwambia jinsi unavyofurahia kuwa naye.
Mwandalie chakula anachopenda
Njia nyingine nzuri ya kumwonyesha mume wako kuwa unamtamani ni kumwandalia chakula anachokipenda. Inaweza kuwa ni chakula maalum ambacho anafurahia au kinywaji kinachomvutia. Anapofurahia chakula hicho, unaweza kutumia nafasi hiyo kumwonyesha upendo na hisisa zako. Kwa mfano, unaweza kumwandalia chakula kizuri mezani na kujaribu kuanzisha mazungumzo ya kimahaba ili kuongeza mvuto kati yenu.