Pambo

SHERIA: Mchakato wa kufanikisha ndoa za kikristo nchini Kenya

Na BENSON MATHEKA May 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAPENZI wanaokusudia kuoana kwa ndoa ya Kikristo huwajulisha  wachungaji au makasisi  wa kanisa lao  nia yao ya kuingia kwenye ndoa.

Mchungaji wa kanisa, pamoja na kamati ya kanisa, hufanya uchunguzi wa awali ili kuthibitisha ikiwa mmoja wa wahusika ni  muumini halali wa kanisa hilo.

Mara baada ya kuridhika kuwa mtu huyo anatimiza vigezo vya kanisa vya kuoa au kuolewa, mchungaji hutangaza kwa mkutano mzima wa waumini kuhusu ndoa hiyo inayokusudiwa na kualika yeyote mwenye pingamizi kuhusu ndoa hiyo kuwasilisha kwa maandishi pingamizi hilo kwake.

Tangazo hili hutolewa mara tatu ili kutoa muda wa kutosha kwa yeyote mwenye pingamizi.Iwapo kuna pingamizi dhidi ya wapenzi hao kuoana, mchungaji aliyepewa leseni atasikiliza na kuamua pingamizi hilo, akipatia pande zote fursa ya kusikilizwa kwa haki ndani ya muda unaofaa.

Ni muhimu kukumbuka kuwa  pingamizi lazima liwe kwa maandishi, lionyeshe uhusiano wa anayepinga na wanandoa watarajiwa, na kueleza misingi au sababu za pingamizi hilo.

Baada ya uamuzi kufanyika, mchungaji au kiongozi wa ibada katika eneo husika ataandaa ripoti kwa maandishi kuhusu mchakato wa uamuzi huo na kuwasilisha kwa Msajili wa Ndoa.

Mtu akikosa kuridhishwa na uamuzi wa mchungaji ana haki ya kukata rufaa mahakamani ndani ya siku 14 baada ya uamuzi huo.

Iwapo hakuna pingamizi au pingamizi limeamuliwa kwa njia chanya, tarehe ya ndoa itawekwa na kutangazwa kwa umma.

Pasta au kasisi anapaswa kuwapa wanandoa watarajiwa ushauri kuhusu maandalizi ya ndoa na mahitaji ya kisheria.

Siku ya ndoa, wanandoa watarajiwa hubadilishana viapo mbele ya mchungaji, familia na marafiki, na waumini wa kanisa.

Mchungaji au kasisi anayeongoza ibada ya ndoa hutia saini cheti cha ndoa na kuhakikisha kuwa pia wanandoa wanafanya hivyo, pamoja na mashahidi wawili.

Baada ya vyeti vya ndoa kutiwa saini na kushuhudiwa, mchungaji au kasisi anayeongoza harusi huwa anahifadhi nakala moja, huwapa wanandoa nakala moja, na nakala nyingine huwasilishwa kwa Msajili wa Ndoa.

Hii inaashiria mwisho wa mchakato wa kufanikisha ndoa ya Kikristo.