• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:19 PM
PAMELA ADHIAMBO: Ari yangu ni kuanzisha kampuni ya uigizaji

PAMELA ADHIAMBO: Ari yangu ni kuanzisha kampuni ya uigizaji

NA JOHN KIMWERE, NAIROBI

ANASEMA akiwa mndogo alidhamiria kuhitimu kuwa mwalimu lakini ingawa alianza kushiriki masuala ya burudani akisoma shule ya Msingi.

Hata hivyo anadokeza kuwa ndoto yake ilimea mabawa mwaka 1995 alipotamatisha masomo ya sekondari kwenye shule ya St Lucy Raruowa Girls Homabay.

Baadaye Pamela Adhiambo alihitimu kwa shahada ya diploma katika masuala ya hoteli za kifahari mwaka 1999. Kisha alifanikiwa kufanya kazi kwa miaka saba kwenye hoteli ya Grand Regency ambayo kwa sasa inafahamika kama Laico Regency Hotel.

Licha ya hayo Pamella amezamia mpango mzima kusukuma guruduma katika tasnia ya maigizo.

Anataka kushiriki uigizaji akilenga kufikia upeo wa kimataifa akifuata nyayo zake mwigizaji wa filamu za Kinigeria (Nollywood) Patience Ozokwor maarufu Mama G.

Kadhalika anasema kuwa anahisi ameiva katika masuala ya maigizo ambapo anapania kuanzisha kampuni yake hivi karibuni ili kuzalisha filamu na kusaidia wasanii wanaokuja kupata kukuza talanta zao.

Mwaka 2013 alijiunga na kundi la Ndio Films Productions ambapo amefanikiwa kushiriki filamu kadhaa tangia enzi hizo.

Ameshiriki filamu nyingi tangu kipindi hicho ikiwamo ‘Mit Billie’ (Tamu ebu onja) iliyopeperushwa kupitia Lolwe TV.

Filamu iliyo ilitegenezwa na Ndio Films Production zingine zikiwa ‘Asali Njungu, ‘Pima Wheight,’ ‘Bila Capital’, zote zimefanikiwa kupeperushwa kupitia K24 TV. ”Kwa sasa chini ya Ndio Film tunaanda filamu mpya inayoitwa ‘Bitter Sugar’ inayotazamiwa kuwa tayari hivi karibuni,” alisema.

Kadhalika anajivunia kushiriki filamu kwa jina Njoro Uber iliyofanikiwa kupeperushwa kupitia Maisha Magic. Chini ya kundi la Charles Omondi Production alishiriki filamu Nairobi Ghost Forest pia wanaandaa filamu inayokwenda kwa jina ‘Stella.’ Pia anashiriki filamu ‘Stuck in the middle’ inayoandaliwa na kundi la Badilisha Production.

Msanii huyu katika uhusika wake kwenye filamu zote alizowahi kushiriki hufahamika kama Mama.

Anasema Wakenya ni wabunifu lakini hawajafanikiwa kupata nafasi nzuri kuonyesha talanta zao katika jukwaa la burundani ya maigizo.

Anaitaka serikali ipunguze ada ambayo hutoza wategenezaji filamu ili kupata kibali cha kunasa video kwenye shughuli zao hali anayosema itavutia wawekezaji wa kigeni hapa nchini.

”Ninaamini endapo serikali inaweza kulegeza kamba kuhusiana na sheria hiyo bila shaka kampuni nyingi za kigeni zinaweza kuvutiwa zaidi kunasa filamu mbali mbali hapa nchini na kutoa nafasi za ajira kwa waigizaji wa humu nchini,” alisema na kuongeza kuwa taifa hili limefurika waigizaji wengi tu ila hawajapata nafasi mwafaka kuonyesha vipaji vyao.

Kando na hayo ndani ya miaka mitano alikuwa anamiliki kampuni ya Palm Criz Tours and Travell akijihusisha na biashara ya teksi ambapo licha ya kubobea kwa kiwango fulani alijikuta njiapanda baada ya wateja kukwepesha magari ya wenyewe.

Kwa sasa ana kesi mbili mahakamani baada ya magari aliyokuwa amekodishia wateja tofauti kuibwa.

”Nilishtakiwa na wenye magari waliokuwa wamenikodishia magari yao,” alisema na kuongeza kuwa hatima yake ni Mungu pekee anayefahamu itakavyokuwa.

Kadhalika anadokeza kuwa aliwahi kupoteza Sh450,000 alizokuwa amewekeza katika mradi uliojulikana kama Deci Pyramid uliozama miaka iliyopita ambapo wanachama wapatao 94,000 walipoteza takribani Sh 2 bilioni.

You can share this post!

JAMVI: Unafiki wa Ruto

Hatutaki kulegeza kamba – Kibera Saints

adminleo