PATA USHAURI WA DKT FLO: Kwa nini anashindwa kustahimili vyakula?
Mpendwa Daktari,
Nitakabiliana vipi na tatizo la mwanangu wa umri wa miaka mitatu kushindwa kustahimili vyakula kadha wa kadha?
Jane, Mombasa
Mpendwa Jane,
Kushindwa kustahimili vyakula kadha wa kadha kwaweza kumaanisha mambo tofauti, ambapo sijui ni aina gani inayomhusisha mwanao. Katika lugha ya kimatibabu, kushindwa kustahimili vyakula kwaweza maanisha matatizo ya kumeng’enya vyakula kadha wa kadha, shida ambayo yaweza sababisha ishara kama vile maumivu ya tumbo, tumbo kuvimba, kuendesha, maumivu ya kichwa, kukohoa, n.k. Mara nyingi hii hutokea mtu anapokosa aina fulani ya kimeng’enya au kutokana na mwasho unaosababishwa na kemikali au uchafu kwenye chakula.
Utambuzi kwa kawaida utafanywa na mtaalamu wa tumbo (gastroenterologist) na tiba inahusisha kuepuka vyakula vinavyomtatiza mwanao kumeng’enya. Shida hii pia inaweza ikaletwa na mzio (allergy) wa aina ya vyakula mbalimbali. Hii inamaanisha kwamba ukila vyakula fulani, mfumo wako wa kinga mwilini unachochewa na hii huenda ikasababisha upele, kamasi kutoka puani, kikohozi, maumivu ya tumbo, kuendesha na kutapika, mtetemeko mkali ambao huenda ukasababisha kifo, vyote kutokana na chakula fulani. Hali hii inadhibitiwa kwa kuepuka aina fulani ya vyakula.
Watoto wadogo pia huenda wakakumbwa na tatizo la kutostahimili aina tofauti ya vyakula kwa sababu wanachagua, na wala sio kutokana na kwamba chakula hicho kinawaathiri kwa njia yoyote. Kufikia miaka mitatu, watoto huwa na maoni yao kuhusu mambo tofauti na wanataka kuyaonyesha ambapo mara nyingi watafanya hivyo kwa kuwa wakorofi na kukataa kula, miongoni mwa mambo mengine. Mojawapo ya maoni yao ni kuhusu rangi au hata mwonekano wa chakula. Kwa bahati mbaya, maoni haya hubadilika kila baada ya siku au wiki kadhaa.
Mojawapo ya sababu ni kwamba kasi yao ya kukua hupungua ikilinganishwa na ilivyokuwa miezi 18 ya kwanza maishani mwao, na hivyo hawahitaji chakula kingi kama ilivyokuwa awali. Jitahidi kukumbatia maoni yao pasipo kupingana naye kila wakati ili wasihusishe wakati wa kula na mvurugano. Kando na hayo, kuwa mbunifu kuhusu jinsi unavyomtayarishia vyakula mbalimbali na ikiwezekana jitahidi kumwandalia kwa njia tofauti ili kumhimiza ale. Aidha, unda mazingira mwafaka ya kula kwa ratiba, epuka vitafunio ambavyo huenda vikalijaza tumbo lake na kumfanya akumbwe na matatizo wakati wa kula chakula.
Mpendwa Daktari,
Mimi ni mwanamume wa umri wa makamo ambapo nakaribia umri wa miaka hamsini. Nimekuwa nikikumbwa na tatizo la kuumwa na tumbo, linaloandamana na kichefuchefu. Nini kinaweza kuwa kinasababisha tatizo hili?
Greg, Nairobi
Mpendwa Greg,
Maumivu ya tumbo na kichefuchefu vyaweza tokana na shida katika ogani yoyote tumboni, ikiwa ni pamoja na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kongosho, figo, mfumo wa kupitisha mkojo au hata mfumo wa uzazi.
Kutambua ni mfumo gani ulioathirika kutategemea na kuwepo au kutokuwepo kwa ishara tofauti, vile vile sehemu hususan inayokumbwa na maumivu.
Kutokana na sababu kuwa tatizo hili limekuwa likikukumba kila mara, litakuwa jambo la busara iwapo utakaguliwa na daktari ambapo uchunguzi unaofaa utafanywa, tatizo hususan kutambuliwa ambapo utatibiwa.