Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nina hofu ya nafasi iliyofungwa, mbona?

February 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Nina tatizo la ‘claustrophobia’ (hofu ya kukaa katika nafasi iliyofungwa au kufunikwa kabisa-(Enclosed space), kwa hivyo mimi hujiepusha na sehemu zilizo na msongamano wa watu. Tatizo hili laweza kuwa lasababishwa na nini, na je, nifanyeje kukabiliana na shida hii?

Alnashir

Mpendwa Alnashir,

Claustrophobia’ ni tatizo linalosababisha hofu kuu mhusika akiwa katika maeneo yaliyo na msongamano wa watu. Ukikumbwa na tatizo hili pengine ukiwa katika chumba kidogo (kama vile kwenye lifti), basi unaonyesha ishara sawa na zile za shambulizi la hofu. Dalili ni pamoja na hofu kuu, kutokwa na jasho jingi, joto, kutetemeka, kichefuchefu, kifua kujikaza, moyo kupiga kwa kasi na kushindwa kupumua. Kwa kawaida ishara hizi hupungua baada ya muda fulani. Kwa watu wengi, hali hii huanza utotoni au katika umri wa kubalehe. Hii yaweza kuwa ni kutokana na tukio la pengine kukwama katika eneo lililofungwa kwa wakati mrefu au bila ridhaa yako (kwa mfano, kuadhibiwa kwa kufungiwa chumbani) au kukumbana na tukio la kuhatarisha maisha, (kama vile mawimbi makali ukiwa kwenye ndege). Aidha, jeni na mabadiliko kwenye ubongo pia huchangia. Kwa kawaida hali hii hudhibitiwa na mtaalamu wa kiafya kwa kutumia tiba ya kiakili. Dawa pia zaweza tumika kukabiliana na ishara za tatizo hili.

 

Mpendwa Daktari,

Ningependa kujua kiharusi ni nini? Je, mgando wa damu ndio husababisha tatizo hili? Je, kiharusi chaweza sababisha kupooza? Pia, ningependa kujua ‘aneurysm’ ni nini?

Walji

Mpendwa Walji,

Kiharusi hutokea sehemu ya ubongo inapokufa hivyo kukosa kufikwa na damu na oksijeni. Hali hii hutokea mishipa ya damu inapozibwa na mgando wa damu (ischemic stroke) au inapopasuka (hemorrhagic stroke). Kwa upande mwingine, shambulio kwa jina transient ischemic attack (TIA) ni aina ndogo ya kiharusi inayosababishwa na kuziba kwa mishipa kwa muda. Ishara ambazo mtu hupata hutegemea na sehemu ya ubongo iliyoathirika. Kwa mfano, ikiwa sehemu ya ubongo inayodhibiti usemi itaathirika, basi mhusika atakumbwa na tatizo la kuzungumza. Ikiwa sehemu ya ubongo iliyoathirika inadhibiti misuli katika sehemu fulani mwilini, basi sehemu hiyo itapooza. Kwa upande mwingine, aneurysm ni sehemu ya mshipa wa damu ambapo kuta zimekuwa nyembamba, dhaifu na kunyooka, suala linalofanya sehemu hiyo iwe rahisi kupasuka. Huenda ukazaliwa na tatizo hili au ukakumbwa nalo baadaye maishani. Baadhi ya mambo yanayokuweka katika hatari ya kukumbwa na hali hii ni pamoja na shinikizo la damu, uvutaji sigara, uzani mzito, kutofanya mazoezi na lishe mbovu. Kwa kawaida, aina nyingi za aneurysm hazisababishi matatizo, lakini miongoni mwa watu wachache, hali hii yaweza sababisha maumivu, damu kuganda na kuvuja damu ndani ya mwili, hali ambazo zaweza sababisha kifo.

 

Mpendwa Daktari,

Nimekuwa na tatizo la mwili wangu kuasha dakika kama kumi hivi baada ya kuoga kwa maji baridi. Nitakabiliana vipi na tatizo hili?

Naliaka

Mpendwa Naliaka,

Unakumbwa na tatizo liitwalo aquagenic pruritus, kumaanisha mwasho unaosababishwa na maji. Ni aina ya mzio wa maji. Kwa kawaida, mgusano

na maji unasababisha mwasho mkali wa ngozi, pasipo kusababisha upele au uvimbe. Ishara zaweza dumu kwa kati ya dakika 10 na masaa mawili, na kwa kawaida tatizo hili huisha lenyewe. Hakuna sababu kuu kuhusu kwa nini baadhi ya watu hukumbwa na hali hii. Lakini wakati mwingine yaweza tokana na matatizo ya damu. Kwa watu wengine, kuoga kwa maji moto huzuia seli (mast cells) zinazochochea mzio huu. Lakini ukioga kwa maji moto sana kwa muda mrefu, huenda ukakumbwa na mwasho kwa sababu ya ngozi kukauka. Unaweza kutumia tembe za kukabiliana na mzio na krimu/ losheni. Usitumie sabuni zenye harufu kali kuoga au kufulia taulo zako. Pia, fua taulo zako kila mara, kwa mfano mara moja au mbili kwa wiki. Hii itasaidia kuzuia kuota kwa bakteria kwenye taulo baridi. Hata hivyo, hali hii haina tiba.