PATA USHAURI WA DKT FLO: ‘Pap Smear’ yatakiwa ifanywe mara ngapi?
Na DKT FLO
Mpendwa Daktari,
Nimekuwa nikitamani kufanyiwa uchunguzi wa ‘Pap Smear’, lakini kutokana na sababu kwamba sina ajira, sidhani kwamba naweza kumudu kufanyiwa utaratibu huu mara kwa mara. Nifanyeje?
Mkazi Mombasa
Mpendwa,
Utaratibu wa pap smear unapaswa kufanywa kila baada ya kati ya miaka mitatu na mitano ikiwa uko chini ya umri wa miaka 45, na mara moja kila mwaka baada ya umri huu ila tu iwapo kuna tatizo. Hii inamaanisha kwamba unaweza kupanga polepole ili kufanyiwa uchunguzi huu. Katika hospitali za umma, uchunguzi huu waweza kugharimu hata Sh100 na katika baadhi ya kampeni za kuhamasisha watu kuhusu kansa, utaratibu hufanywa bila malipo.
***
Mpendwa Daktari,
Rafiki yangu husafisha koo kila mara. Tatizo laweza kuwa nini?
Evelyne, Nairobi
Mpendwa Evelyne,
Kusafisha koo kila mara kwaweza kusababishwa na mambo kadha wa kadha. Kunaweza kutokana na hali inayofahamika kama post-nasal drip ambapo kamasi hutiririka kwa kuelekea chini ya koo na hivyo kusababisha mwasho. Hii pia yaweza kuwa kutokana na mzio unaoathiri pua au uwazi katika mfupa wa fuvu unaowasiliana na mianzi ya pua (sinuses). Aidha, kusafisha koo kunaweza kutokana na laryngopharyngeal reflux (LPR) ambapo chakula tumboni kinarejea kwenye umio na kusababisha mwasho na hata kumwagika kwenye njia ya hewa na kuathiri sauti. Maradhi ya pumu, mkamba (bronchitis) na mapafu yaweza kusababisa mwasho wa koo kutokana na kikohozi cha muda mrefu. Pia hali hii yaweza kusababishwa na matumizi ya kivutia hewa (inhalers).
Aidha kuna baadhi ya dawa ambazo zaweza kusababisha mwasho wa koo ambapo mhusika anahisi kana kwamba kitu kimekwama au kikohozi kimemkaba shingoni. Kuna baadhi ya dawa zinazotumika kukabiliana na shinikizo la damu au mfadhaiko ambazo huchochea hali hii.
Pia tatizo hili laweza kutokana na wasiwasi, kukaukiwa maji mwilini na kukazika kwa sauti. Ukiwa na wasiwasi kuhusu tatizo fulani, basi misuli ya koo hukazika na kusababisha hisia za kusakamwa. Hii ndio sababu watu wengi husafisha koo zao au kujaribu kulegeza mavazi shingoni wakikumbwa na wasiwasi.
Hata hivyo unapaswa kufahamu kwamba jinsi unavyozidi kusafisha koo yako ndivyo unavyozidi kusababisha mwasho, suala linalokufanya uhisi kana kwamba unataka kukohoa zaidi.
Sababu kuu ya tatizo hili ni maambukizi, au mzio. Kumbuka kwamba kila mtu huzalisha kamasi nyuma ya koo mara kwa mara na kumeza bila kujua. Kwa upande wa wanaosafisha koo zao, tatizo ni kwamba wanahisi hili linapofanyika. Ushauri wangu ni kwamba upate ushauri wa mtaalamu wa ENT kukabiliana na hali hiyo.
***
Nimekuwa na mazoea ya kuangalia watu vinywani kubaini ikiwa wana ukuvu wa mdomoni (oral thrush). Hii ni mbinu yangu ya kutafuta wachumba kwani hii hunipa kidokezi cha iwapo mtu ana virusi vya HIV. Kuna matatizo mengine ya kiafya yanayosababisha hali hii?
M.M., Nairobi
Mpendwa M.M.,
Mbinu pekee na ya uhakika kujua hali ya HIV ya mwenzako ni kwa kupimwa. Mtu anapoambukizwa virusi vya HIV, anaweza kudumu kwa kati ya miaka minane na kumi kabla ya kuanza kuonyesha ishara zozote.
Aidha, wale wanaopokea matibabu na viwango vya virusi hivi mwilini viko chini, hawatakumbwa na maambukizi kama ukuvu wa mdomoni. Kumbuka kwamba maradhi yoyote yanayoathiri kingamwili ya mhusika yaweza kumfanya mtu kukumbwa na ukuvu wa mdomoni. Hii ni pamoja na HIV, kisukari, maradhi ya figo, matatizo ya kihomoni, kansa, uzee, umri mdogo sana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli na za kutibu kansa.