Makala

PATA USHAURI WA DKT FLO: Sina mimba, lakini nahisi kichefuchefu

March 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na DKT FLO

NIMEKUWA nikikumbwa na kichefuchefu kwa kipindi cha wiki tatu sasa. Nilifanyiwa uchunguzi wa ujauzito na kupatikana kwamba sina mimba. Tatizo laweza kuwa lipi na nitakabiliana nalo vipi?

Cate, Mombasa

Mpendwa Cate,

Kichefuchefu kwa kawaida huandamana na matatizo ya tumbo na hisia za kutaka kutapika. Huenda hali hii ikadumu kwa muda mfupi kisha kurejea mara kwa mara, au ikadumu kwa muda mrefu. Huenda hali hii ikachochewa na mambo mbali mbali ikiwa ni pamja na baadhi ya vyakula au harufu, maambukizi ya mfumo wa utumbo, vidonda vya tumboni, aina tofauti za dawa, kula chakula kingi, msongo wa akili, kunywa pombe kupindukia, mzio wa vyakula, ujauzito, kuumwa na kichwa, utumbo kuziba, maumivu kutokana na viungo vilivyo karibu na tumbo kwa mfano kutokana na ugonjwa wa kidole tumbo (appendicitis), maradhi ya kibofu, maradhi ya kongosho, homa ya uti wa mgongo (meningitis), matatizo kwenye ubongo, miongoni mwa amambo mengine mengi.

Itakuwa vyema kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu wa kina ili kubaini nini hasa kinachokusababishia matatizo haya ili upate tiba inayokufaa.

Ili kuzuia kichefuchefu, kula viwango vidogo vidogo vya vyakula badala ya viwango vikubwa, kula polepole, baada ya kula hakikisha sehemu ya juu ya mwili wako imeinuka kwa kukaa au kusimama; usinywe maji wakati wa kula; jiepushe na mazoezi au shughuli zito baada ya kula chakula kingi; jiepushe na vyakula ambavyo ni vigumu kumeng’enya au vinavyochochea zaidi kichefuchefu kama vile vyakula vilivyopikwa kwa viuongo vingi au vilivyo na mafuta mengi, kula vyakula vilivyopashwa moto badala ya baridi. Pia, unapohisi kichefuchefu, unaweza kujizuia usitapike kwa kupumzika huku sehemu ya juu ya mwili wako ikiwa imeinuka, vile vile kwa kunywa viwnago vidogo vidogo vya maji.

 

Ningependa kujua zaidi kuhusiana na virusi vya corona ili nijue jinsi ya kuilinda familia yangu endapo kutakuwa na mkurupuko nchini. Nahitaji taarifa kuhusu hatari, nini kinachosababisha, dalili, jinsi ya kuzuia, tiba ikiwa ipo, vile vile uwezekano wa kufariki endapo nimeambukizwa.

Vivian, Nairobi

Mpendwa Vivian,

Virusi vya corona ni jamii kubwa ya virusi vinavyosababisha maradhi kama vile mafua na hata ugonjwa wa mfumo wa kupumua. Virusi hivi vinasambaa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu. Maradhi ya sasa yanayosababishwa na virusi vya corona yanafahamika kama Covid-19.

Maradhi haya hayakuwa yanatambulika kabla ya mkurupuko eneo la Wuhan, nchini China kutajwa mnamo Februari 11, 2020. Kutokana na suala hili, utafiti bado unaendelea ili kujifunza mengi kuhusiana na virusi hivi.

Baadhi ya watu wanaoambukizwa virusi hivi kwa kawaida hawaugui kamwe. Takriban asilimia 80 ya watu hupata ishara ndogo ambazo hazihitaji matibabu maalum. Ishara zinazojitokeza kwa wingi ni pamoja na homa, uchovu na kikohozi kikavu. Huenda mgonjwa pia akakumbwa na ishara zingine kama vile kutokwa na kamasi, pua kuziba, maumivu ya koo na kuendesha.

Takriban asilimia 16 ya walioambukizwa huugua sana maradhi ya nimonia mbali na kukumbwa na matatizo ya kupumua. Kufikia sasa, idadi ya vifo vinavyosababishwa na virusi hivi ni takriban 2%, japo viwango hivi vyaweza kuwa juu au chini katika sehemu tofauti. Wale walio katika hatari kubwa ya kuugua sana kutokana na virusi hivi ni wazee na wale walio na maradhi kama vile kisukari, shinikizo la damu na maradhi ya moyo.

Virusi hivi husambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia vitone vinavyotapakaa mtu aliyeambukizwa anapokoa, kupiga chafya au kupumua. Huenda vitone vikavutwa moja kwa moja na mtu ambaye hajaambukizwa, au huenda vikaangukia vifaa au sehemu ambazo mtu ambaye hajaambukizwa atagusa kisha kushika macho, mdomo au pua, na hivyo kuambukizwa.

Mbinu za kuzuia maradhi haya ni pamoja na kunawa mikono au kujipangusa mikono kwa kutumia dawa maalum ya kupambana na vijidudu, kutogusa macho, pua na mdomo; kufuata taratibu za usafi kama vile kukohoa/kupiga chafya kwenye kitambaa (kisha ukioshe), karatasi ya shashi, au kiwiko.

Unashauriwa kukaa umbali wa angalau mita moja na mtu anayekohoa au kupiga chafya ili usivute vitone vinavyotapakaa anapofanya hivyo. Wale ambao tayari wameambukizwa wanapaswa kukaa nyumbani na kupunguza kuingiliana na watu wengine. Kabla ya kuzuru kituo cha afya, piga simu kwanza kisha ufuate masharti utakayopewa. Kuna dawa na chanjo zinazofanyiwa uchunguzi, japo wengi wa walioambukizwa wamepona kutokana na huduma nzuri.