Makala

Patrick Mukanga: Mtangazaji, mwalimu na mshauri wa lugha

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na PETER CHANGTOEK

Patrick Michael Mukanga ni mja mwenye vipaji vingi. Yeye ni mtangazaji, mwalimu, mwandishi wa vitabu na pia mshauri na hutoa nasaha kuhusu masuala ya lugha za Kiingereza na Kiswahili.

Alizaliwa mnamo mwaka 1990, katika kitongoji cha Bujwang’a, kaunti ndogo ya Butula, Kaunti ya Busia.

Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi ya Khunyangu, iliyoko katika Kaunti ya Busia, mnamo mwaka 1996, kabla hajajiunga na nyingine ijulikanayo kama St. Teresa Nelaa, akiwa katika Darasa la Nne, alikofanyia mtihani wa KCPE, mnamo mwaka 2005.

“Baadaye, nikajiunga na shule ya Upili ya Lugulu A.C, kuanzia mwaka 2006 hadi 2007. Mnamo mwaka 2008, nililazimika kukaa nyumbani kwa sababu ya kukosa karo,” afichua Mukanga.

Huku akiwa nyumbani baada ya kukosa karo, alishurutika kujihusisha na shughuli ainati za kilimo, ili apate hela za kulipia karo.

Juhudi zake zilimlipa. Baada ya kuyauza baadhi ya mazao ya shambani, alijiunga na shule tofauti mnamo mwaka 2009, ili kuyaendeleza masomo yake.

“Mnamo mwaka 2009, nilijiunga na St. Mathias Secondary School, Busia, kuanzia Kidato cha Tatu hadi cha Nne, na kufanya mtihani wa KCSE mwaka 2010,” asimulia Mukanga, mwenye umri wa miaka 30.

Mnamo mwaka 2011, baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya upili, aliendeleza shughuli za kilimo.

“Mnamo Mei, 2012, nilijiunga na Kenya Institute of Media and Technology, iliyokuwa katika Taveta Road, Nairobi, ambapo nilisomea diploma katika kozi ya uandishi wa habari na utangazaji,” adokeza Mukanga, ambaye alikamilisha masomo hayo mwaka 2014.

Mnamo Juni, 2014, alijiunga na Around The Globe (ATG) Radio, ili kuhudumu kwa mafunzo ya nyanjani, kwa kipindi cha miezi miwili. Baada ya muda huo kukamilika mnamo Agosti mosi, aliajiriwa kuko huko, kwa muda wa mwezi mmoja, ambapo alikuwa akichukua na kuzihariri video zilizokuwa zikitumiwa katika runinga ya Deliverance TV, inayomilikiwa na shirika la habari la ATG.

Mnamo Septemba, 2014, alijiunga na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), ili kupata mafunzo mengine ya nyanjani, hadi Disemba. Akiwa kule, alipata fursa ya kufanya kazi na akina Charles Otunga, Kennedy Epalat, Franco K. Lusaka, miongoni mwa wengine.

Mbali na kukiandaa kipindi cha Darubini, Mukanga pia alikuwa ametwikwa jukumu la kuziandika na kuzisoma habari, katika Radio Ingo, iliyokuwa ikimilikiwa na KBC.

Hata hivyo, kipaji chake kilianza kuonekana mapema, akiwa katika shule ya msingi ya Nelaa, na hata mwalimu wake mmoja akamwambia kuwa, angekuwa mwanahabari baadaye.

“Nilikuwa nikiwaiga watangazaji kama vile Charles Otunga, Hassan Ali (Radio Maisha), marehemu Waweru Mburu na Mohamed Ali,” asema Mukanga, ambaye ni mzawa wa saba, katika aila ya watoto kumi na wawili.

Anasema kuwa alianza kuandika alipokuwa katika Kidato cha Kwanza. Hata hivyo, hajaanza kuichapisha mingi ya miswada yake.

Kwa sasa, amekichapisha kitabu kimoja, Mwerevu Mjinga, kilichochapishwa na Onmove Publishers. Alikiandika kitabu hicho kwa kuutumia mwangaza wa mshumaa.

Kitabu hicho kinamhusu kijana mmoja anayejulikana kama Mworia, ambaye ni mhusika mkuu, aliyekuwa mwerevu darasani, ila akaja kunaswa kwenye ulimbo wa mihadarati.

Alikuwa na miswada kumi na mitatu, lakini ameuchapisha mmoja, na ana kumi na miwili iliyosalia. Anaongeza kuwa aliliona pengo katika uandishi wa vitabu vya watoto, na akaamua kulijaza

Mbali na kuwa mtangazaji na mwandishi wa vitabu, Mukanga pia ni mshauri wa lugha za Kiswahili na Kiingereza, si tu katika shule za msingi, bali pia katika shule kadha wa kadha za sekondari.

Miongoni mwa shule ambazo amewahi kuzuru na kuwapa wanafunzi nasaha ni: Kids Village Academy (South C), Nairobi South Primary School (South B), Winka Academy (South C).

Pia, amewahi kutoa nasaha na mwongozo katika shule kadhaa za upili nchini, zikiwamo BDS Secondary School (Industrial Area), Kingandole Secondary School (Busia) na Bukhalalire Secondary School (Butula).

Mwandishi huyo anawasihi wale ambao wana azma ya kujiunga na uanahabari kuwa na mtazamo na kutositasita. Isitoshe, Mukanga anawashauri kufanya utafiti, na kukumbuka kuwa hakuna ndoto yoyote ambayo itatimia, endapo mja hatatia bidii za mchwa.

Anaazimia kupata masomo ya juu, hususan ya lugha ya Kiswahili. Aidha, ananuia kushirikiana na waandishi wengineo wenye tajriba pana, kuviandika vitabu, katika siku za usoni.