Makala

PHANE KERUBO: Lengo langu ni kumfikia Jennifer Lopez

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NDIO anaelekea kutinga miaka minane tangu aanze kujituma katika masuala ya uigizaji ambapo amepania kufikia kiwango cha wasanii wa hadhi ya Hollywood.

Anasema kando na hayo pia anadhamiria kumiliki brandi ya kuzalisha filamu ili kukuza waigizaji wanaokuja.

Binti huyu, Phane Kerubo Mecha ni mwigizaji, mwaandishi wa scripts pia kushuti video za filamu. Ingawa amezamia katika masuala ya uigizaji amehitimu kwa shahada ya diploma katika taaluma ya uanahabari.

”Binafsi napenda kuigiza maana tangu nimalize masomo ya uanahabari nimekuwa nikishiriki maigizo,” anasema na kuongeza kuwa anajivunia kuigiza zaidi ya filamu kumi.

Chipukizi huyu anasema ingawa tangu akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa daktari alivutiwa na uigizaji mwaka 2011 alipotazama filamu ya ‘Blood Sisters’ ya msanii Genievive Nnaji aliye kati ya wana maigizo mahiri wa Kinigeria (Nollywood).

Katika mpango mzima demu huyu anasema amepania kufikia kiwango chake mwigizaji mahiri nchini Marekani, Jennifer Lynn Lopez ambapo huvutiwa zaidi na filamu yake iitwayo ‘Anaconda.’

Msanii huyo ameigiza filamu nyingi ikiwamo: ‘Hustlers,’ ‘Second Act,’ ‘Maid in Manhattan,’ ‘Enough,’ ‘Selena,’ na ‘The Wedding planner,’ kati ya zingine.

Kerubo anajivunia kuigiza filamu kadhaa ambazo zimefanikiwa kupata mpengo kupeperushwa kupitia runinga tofauti hapa nchini ikiwamo: ‘Hekaya za Likobe (QTV),’ ‘Kelele FM (K24 TV),’ ‘Daktari (KTN TV),’ ‘Kijakazi chizi (Star Times Swahili),’ ‘Hullabaloo (Maisha Magic East),’ na ‘Aunty Boss (NTV Televisheni),’ kati ya zingine.

Anajivunia kushiriki filamu kama ‘Kijakazi chizi,’ ‘Wacha kulenga,’ ‘Trapped in the past,’ ‘Kiherehere,’ ‘Majirani,’ ‘Kelele FM,’ ‘Majuto,’ ‘Varshita,’ ‘Hekaya za likobe,’ kati ya zingine.

Mwana maigizo huyu amefanya kazi na makundi mbali mbali ya kuzalisha filamu ikiwamo Tamasha Arts Production, Moon Beam Production, Shoe Back Group na Phil It production kati ya mengine.

Mwigizaji huyu anasema kwa waigizaji wa humu nchini angependa sana kufanya kazi na Catherine Kamau (Mother in law pia Sue and Johnny) bila kuweka katika kaburi la sahau Brenda Wairimu (Monica pia Lies that Bind) kati ya wengineo. Kwa waigizaji mahiri barani Afrika anasema anatamani kufanya kazi na wanamaigizo kama Mercy Johnson na Funke Akidelle wote wazawa wa Nigeria.

Anaponda maprodusa wa Kenya kwa kutokuwa wabunifu kwenye juhudi za kuzalisha filamu zinazoangazia utamaduni wa taifa hili ili kuvutia watazamaji wa humu nchini. ‘

‘Bila kuwapigia chini maprodusa wetu ndio huchangia wakenya wengi kupenda kutazama filamu za kigeni,” alisema na kutoa mwito kwao wawazie suala hilo ili kuinua tasnia ya filamu nchini.

Binti huyu kamwe sio mchoyo anashauri wenzake wanaoibukia kuwa wavumilivu na kufanya kazi ya uigizaji kwa kujitolea hata wakipata nafasi gani. Anawaambia kuwa kujituma kwao kutachangia watambulike wanatosha mboga katika maigizo.