Pigo kwa wanyamapori Tsavo mhisani wa kuwapa maji wakati wa ukame akifariki
PATRICK Kilonzo Mwalua, maarufu kama “Mnyweshaji wanyamapori wa Tsavo,” alifariki asubuhi ya Jumanne akiwa na umri wa miaka 51 baada ya kupambana na matatizo ya figo kwa miaka 10.
Bw Mwalua alifariki nyumbani kwake katika kijiji cha Kajire, Kaunti ya Taita Taveta, alipokuwa akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Moi huko Voi kwa ajili ya kusafishwa figo.
Bw Mwalua anafahamika kimataifa kwa juhudi zake za uhifadhi, ambazo zilimpa sifa duniani, ikiwa ni pamoja na tuzo ya Rais na Uwadeni wa Heshima, miongoni mwa nyingine nyingi.
Ushirikiano wake katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira utabaki alama kubwa haswa katika eneo la Tsavo.
Mnamo 2016, wakati wa msimu mrefu wa ukame, akiwa mkulima katika kijiji chake cha Kajire, alishuhudia matokeo mabaya ya mabadiliko ya tabianchi kwa wanyamapori.
Kwa upendo mkubwa kwa wanyama pori, alianzisha kampeni ya kunywesha wanyamapori maji katika maeneo mengi ya mbuga ya Tsavo ili kuzuia vifo vya wanyama.
Akiongea na Taifa Leo, Mke wake, Rachel Kilonzo, alisema kuwa yuko tayari kuendeleza kazi yake ya uhifadhi.
Alitaja juhudi zake kuwa zilikuwa za kishujaa.
“Bidii yake ilikuwa ya kuigwa. Tutamheshimu na kumuenzi kwa kuendelea kulinda wanyamapori na juhudi zake za kutunza mazingira,” alisema.
Alisema licha ya ugonjwa wake, alihakikisha kuwa miradi yake ilikuwa inaendeshwa kwa manufaa ya jamii na wanyamapori.
“Hata wakati hakuweza kutembea, alifuatilia miradi yake kupitia simu. Kama familia juhudi zake ni za kuigwa,” alisema.
Kifo cha Bw Mwalua kimeathiri sana jamii yote kwa ujumla. Licha ya migogoro ya mara kwa mara kati ya binadamu na wanyamapori, Mwalua aliwahimiza wenyeji kupanda mazao ambayo hayavutii ndovu na hivi kuleta uwiano.
Alianzisha mipango mbalimbali ya kilimo na kuwahamasisha na kuwasaidia wakulima wengi katika eneo lake kukumbatia teknolojia mpya za kilimo.
Katika siku zake za mwisho, hata alipokuwa anakabiliana na matatizo ya figo, alitafuta mashine ya kukamua mafuta ya alizeti ili kuwasaidia wakulima kutoka jamii yake.
Msemaji wa familia, Jones Chengo, alisema maandalizi ya mazishi yanaendelea nyumbani kwake Kajire, alipokuwa akiishi.
“Naomba serikali na mashirika yote yaliyoshirikiana na marehemu kutusaidia katika kusitiri mwili na vilevile kuendeleza juhudi zake za uhifadhi,” alisema.