Makala

Polisi sita watetewa kumuua mshukiwa wa wizi wa sh72 M za benki

Na RICHARD MUNGUTI October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKUFUNZI wa maafisa wa polisi katika chuo cha Kigango amewaondolea lawama maafisa sita wa polisi wanaoshtakiwa kwa kumuua mshukiwa mkuu katika wizi wa Sh72milioni za Benki ya Standard Chartered mnamo Machi 2020.

SSP Dennis Omunga alimweleza Jaji Margaret Muigai anayesikiza kesi dhidi Koplo Joseph Ojode Obambo, Konstebo (Konst) Henry Mutai, Konst Bashir Ali, Konst Charles Kirimi, Inspekta James Ingige na Koplo Vincent Odhiambo kwamba walimuua Wycliffe Vincent Owuor wakijikinga.

SSP Omunga alisema washtakiwa hao walimwagiza Owuor na wenzake wawili wasimame na kutupa chini silaha walizokuwa nazo lakini wakakaidi na “badala yake wakawafyatulia risasi.”

Jaji Muigai aliambiwa Owuor aliyekuwa na bastola ya kujitengenezea na kisu aliwafyatulia risasi maafisa hao sita wa polisi.

“Polisi hawa waliwakabili Owuor na wenzake wawili. Owuor alipigwa risasi akafa papo hapo lakini wenzake wawili walitoroka kwa Pikipiki huku wakifyatua risasi angani,” SSP Omunga alisema.

SSP Omunga ambaye Mei 24 2020 alikuwa afisa mkuu (OCS) kituo cha polisi cha Kayole alikii kwamba ni yeye aliwatuma maafisa hao sita kukabili washukiwa waliokuwa wanatekeleza wizi katika biashara moja kwenye Kayole Junction.

“Nilipokea taarifa kwamba kulikuwa na wizi unaotekelezwa katika Kayole Junction na wezi waliokuwa wamejihami kwa mabastola. Niliwaagiza maafisa sita wa polisi wakimbie kuzima wizi huo,” SSP Omunga alisema.

Maafisa hao walienda katika biashara iliyokuwa inalengwa kuibwa na kuwaagiza washukiwa hao wajisalamishe lakini walikaidi.

“Badala ya kusimama na kujisalimisha washukiwa hao waliwafyatulia polisi risasi. Polisi waliwakabili na kumpiga risasi Wycliffe Vincent Owuor,” alisema SSP Omunga.

Wakili Danstan Omari (kulia) na afisa mkuu wa polisi SSP Dennis Omunga katika mahakama kuu ya Milimani. Picha| Richard Munguti.

Mahakama ilielezwa wenzi wawili wa Owuor walitoroka kwa piki piki huku wakipiga risasi angani.

Mahakama ilielezwa bastola ya kujitengenezea na kisu vilipatikana na Owuor.

Bastola hiyo iliwasilishwa kama ushahidi kortini.

Afisa huyo akihojiwa na wakili Danstan Omari anayewatetea maafisa hao wa polisi alifichua kwamba “Kayole ni eneo ambapo uhalifu uko juu mno.”

Alisema alipokuwa OCS Kayole 2020 kila siku watu walikuwa wananyang’anywa na kuporwa mali zao.

“Maafisa 13 wa polisi waliuawa na wezi katika kipindi kile nilikuwa OCS Kayole,” alifichua SSP Omunga.

Afisa huyo wa polisi alidokeza kuwa miongoni mwa maafisa wakuu waliouawa ni pamoja na afisa wa kikosi cha kumlinda Rais.

“Maafisa 13 wa Polisi walioua na majambazi Kayole waliporwa silaha zao,” SSP Omunga alifichua.

Jaji Muigai alielezwa “maafisa wa polisi walichukulia Kayole kuwa “kinyonga” mahala pa kufika maafisa wa kulinda usalama.”

Kesi hiyo itaendelea Feburuari 26,2026.

Alipokufa Owuor alikuwa nje kwa dhamana ya Sh500,000 katika kesi hiyo ya wizi wa Sh72milioni.