Prince Indah atoa wimbo wa kumwomboleza Raila
MWANAMUZIKI maarufu Evans Ochieng Owino anayefahamika sana kama Prince Indah ametoa wimbo mpya wa kumwomboleza Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga.
Kupitia wimbo huo Tribute to RT. Hon Raila Odinga alioutoa saa saba zilizopita, Indah anamsifu sana Bw Odinga huku akimrejelea kama shujaa ambaye ameleta mabadiliko makubwa nchini.
“Apenjo, kara iwewa gi ng’awa, dwoka kiwinja Baba (Nauliza, unatuacha na nani Baba, naomba unijibu ikiwa unanisikiza),” Indah anasema katika wimbo huo.
Kwa upande mwingine, mwanamuziki huyo mashuhuri anasema kuwa Bw Odinga alileta demokrasia nchini na kupigania haki za wanyonge.
“Kata Gen-Z bende yuaka (Hata vijana wa Gen Z wanaomboleza kifo chako).”
“Piny yuak. Kata ka Nyasaye otimo dwache, matolit jothurwa (Dunia inaomboleza. Habari hii inauma).”
Watu zaidi ya 164,651 wamesikiza wimbo huo.
Indah ameonekana mara kadhaa akiwa na Bw Odinga wakifurahia nyimbo za mwanamuziki huyo.
Bw Odinga alifariki dunia Jumatano asubuhi Oktoba 15, 2025 huko Koothattukulam, wilayani Ernakulam nchini India, baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati anafanya matembezi yake ya kila asubuhi, kulingana na polisi na viongozi wa hospitali.

Odinga, mwenye umri wa miaka 80, aliangua wakati wa matembezi ya asubuhi ndani ya uwanja wa kituo cha tiba ya Ayurveda, na alikimbizwa Hospitali ya Macho ya Sreedhareeyam Ayurvedic na Kituo cha Utafiti huko Koothattukulam, ambapo alitangazwa kuwa amefariki dunia, msemaji wa hospitali hiyo alisema.
Kando na Indah, wanamuziki wengi akiwemo Bahati wametoa nyimbo za kumwomboleza Bw Odinga wakimtaja kama kiongozi mashuhuri na mtetezi wa demokrasia.
Katika miaka ya hivi karibuni, Indah ameinuka kwa kiwango kikubwa katika tasnia ya muziki. Alianza kuimba kwenye bendi ya R.O.R iliyokuwa ikimilikiwa na Emma Jalamo kabla ya kuwa msanii huru.
Mwaka 2014 alirekodi albamu yake ya kwanza iliyokuwa na nyimbo 6 ambazo ni pamoja na Cinderella, Nyakisumu, Pokna, Uchumi na Ken Soldier.
Oktoba 2016, Prince Indah alirekodi albamu ya pili aliyoipa jina ‘Tenda Wema’ aliyozindua rasmi Desemba 23 mwaka huo.
Baada ya hapo aliondoka kwenye bendi ya R. O. R na kuunda yake Malaika Ohangla Rhumba – M.O.R.