Makala

Raha ya wakazi ujenzi wa ukuta ukiwapa matumaini ya kuepuka dhoruba za bahari

Na KALUME KAZUNGU January 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa kijiji cha Mbwajumwali, Kaunti ya Lamu, sasa wana matumaini ya kuepuka hasara wakati wa dhoruba kali baharini.

Hii ni baada ya ujenzi wa ukuta wa ufukweni kuanzishwa.

Ukuta aina hiyo kwa kawaida hujengwa kwenye ufuo wa bahari ili kuzuia maji kutoka baharini kufikia makazi ya binadamu.

Kijiji cha Mbwajumwali ni makazi ya karibu watu 3,000, ambapo wengi wao hutegemea uvuvi kama kitega uchumi.

Gavana wa Lamu, Issa Timamy akizunguka kijiji cha Mbwajumwali, Lamu Mashariki akiwa na wananchi. Alizindua ujenzi wa ukuta wa ufukweni eneo hilo. Picha|Kalume Kazungu

Kila mara kunapokuwa na dhoruba kali na bahari kujaa , maji husomba makumi ya nyumba kijijini.

Serikali ya Kaunti ya Lamu sasa imezindua mradi wa ujenzi wa awamu ya kwanza ya ukuta huo wa mita 300 ufuoni kwa gharama ya Sh25 milioni.

Gavana Issa Timamy alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika Juni 2025.

“Tumesikia kilio cha muda mrefu cha wakazi hapa Mbwajumwali. Ukuta wenyewe utajengwa kwa mbinu ya kisasa, hivyo kuzuia kabisa maji ya Bahari Hindi kufikia makazi ya binadamu,” akasema Bw Timamy.

Sehemu mojawapo ya kijiji cha Mbwajumwali bila ukuta wa ngome ya ufukweni. Picha|Kalume Kazungu

Afisa Mkuu Msimamizi wa Idara ya Barabara, Uchukuzi, Miundomsingi na Ujenzi, Bw Alex Katana Jimbi, alisema mbali na ukuta huo kuzuia maji ya Bahari Hindi kufikia nyumba za wakazi, pia utasaidia wavuvi kutia nanga mashua zao wakati wanapotoka au kuingia baharini.

Alimsisitizia mwanakandarasi kuharakisha ujenzi ili wananchi wafaidi mapema.

“Ujenzi wa ukuta huu ukikamilika tutakuwa tumesuluhisha matatizo ya karibu miaka 800 iliyopita,” akasema Bw Jimbi.

Bw Mohamed Bakari, mkazi, alisema yeye binafsi na familia yake walilazimika kuhamia kwingine kutokana na boma lao kusombwa kila mara na maji ya Bahari Hindi.

Ukuta au ngome ya ufukweni eneo la Mokowe, Lamu Magharibi. Picha|Kalume Kazungu

“Kukosekana kwa ukuta wa ufukweni ni taabu. Bahari inapofura karibu mara mbili ya kila mwezi nyumba zetu hapa Mbwajumwali husombwa na maji. Nafurahia kwamba ujenzi unaonuiwa utazuia shida tunazoshuhudia kila mara hapa kwetu,” akasema Bw Bakari.

Vijiji vingi vya Lamu Mashariki ni visiwa ambavyo vimezingirwa na Bahari Hindi, hivyo ni muhimu kujengewa ukuta wa ufuoni.
Mbali na Mbwajumwali, vijiji vingine ambavyo tayari vimejengewa kuta za ufukweni ni Pate, Faza, Kizingitini, Mkokoni, Ndau na viunga vyake.