RIZIKI: Ameuza sketi kwa zaidi ya miaka 10
Na SAMMY WAWERU
ISEMWAVYO utamu wa kazi ni pesa, kwa Zipporah Ndereba utamu wa biashara ni kuuza sketi, mavazi maalum ya jinsia ya kike.
Zipporah ambaye ni mama ya watoto wawili ana tajiriba ya uuzaji wa nguo hizo kwa zaidi ya miaka 10.
“Sikuanza biashara ya kuuza sketi leo, wala jana wala juzi, niliianza hata kabla ya Thika Superhighway kuanza kuundwa,” adokeza mfanyabiashara hiyo. Ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha mji wa Thika na mitaa kadha iliyoko viungani mwa jiji la Nairobi ulianza 2009.
Zipporah anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba awali alikuwa karani wa kampuni moja ya ulinzi jijini Nairobi.
Shinikizo la kuingilia biashara lilijiri kupitia mama rafikiye, anayeeleza biashara ya uuzaji nguo ilimuinua kwa kiwango kikubwa.
“Wakati nikilalamikia madeni kila mwisho wa mwezi, alikuwa mmoja wa waliokuwa wakinikopesha,” Zipporah anasema. Mama huyo na ambaye kwa sasa angali katika sekta ya biashara, Zipporah anasema aliuza mavazi ya jinsia kike, watoto, pamoja na malazi kama vile ‘duvet’ na mashuka.
Kulingana na Zipporah, mama wa wavulana wawili, miaka minane na mitano, mshahara wake ulikuwa chini ya Sh15,000 kwa mwezi. Baada ya kuhangaika si haba kukimu mahitaji ambayo yalizidi kwa kiwango kikuu pato lake, mwishoni mwa 2007 aliamua kuchukua hatua nyingine.
“Niliamua liwalo na liwe sitaendelea kuwa mtumwa wa kazi ya madeni mwishoni mwa mwezi. Isitoshe, niliitwa ‘mama ombaomba’ na ni jambo lililoniuma,” Zipporah akumbuka.
Mwanzoni mwa 2008 kwa mtaji wa Sh5,000 pekee mama huyo alienda katika soko maarufu la Gikomba, lililoko jijini Nairobi akanunua sketi na kuanza biashara.
Anasema alianza kwa njia ya uchuuzaji. Kwa mujibu wa maelezo yake, siku ya kwanza hakuuza chochote, suala lililomshtua “nimetoka kwenye kikaango nikaingia motoni”.
Siku ya pili, mkondo ulikuwa uleule, waliteja wakiahidi kumnunulia siku nyingine.
Zipporah anasema nusra afe moyo, na ni katika harakati hizo yule mama kielelezo chake alimshawishi atangamane na wateja, akiomba kujua aina ya sketi walizotaka.
Siku ya tatu, Zipporah anasema alivalia njuga wazo hilo na ambalo siku ya nne lilionekana kuzaa matunda.
“Nilifanya mauzo ya sketi saba,” afichua.
Akiwa amenunua moja kwa Sh50 alikuwa akiiuza Sh150 hiyo ikiwa na maana kuwa alipata faida ya Sh700.
Mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi Jackson Kamau anasema ili kufanikisha biashara, ni muhimu mfanyabiashara kuelewa bayana mahitaji ya soko analolenga.
“Kabla kuingilia biashara yoyote ile, na hata kilimo, ni busara kufanya utafiti wa kina kujua soko la bidhaa au mazao yako ni gani na kinachokosa,” ashauri mtaalamu huyo.
Kwa mtangulizi, ni hatua anayosema anapaswa kufanya ziara katika masoko au eneo na kutangana na wafanyabiashara na wenyeji.
“Pia, kuna biashara zinazoendelea lakini haiafikii mahitaji ya wateja, ukijiri na wazo tofauti na bora, utawahi kiu cha wateja,” Kamau asema.
Zipporah Ndereba anasema baada ya kuelewa mahitaji ya wateja wake, biashara hiyo ilishika kasi. Isitoshe, alipanua mawazo na kulenga vituo vya matatu hasa majira ya jioni.
“Huo ndio wakati wengi hutoka kazini,” aeleza.
Baada ya Thika Superhighway kukamilika, mama huyo alijiunga na wafanyabiashara wengine kutafuta nafasi maalum kusukumia gurudumu la maisha eneo la Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi. Anaendeshea shughuli hiyo pembezoni mwa steji ya matatu yanayohudumu kati ya mtaa huo na Nairobi, ambapo kuna soko maarufu la Jubilee. Amejenga kibanda.
Sketi anazouza ni za muundo halisi wa mavazi yanayohitaji katika nyingi ya ofisi. Wakati wa mahojiano alisema bei yake ni kati ya Sh150 – 400. Alisema biashara hiyo hunoga mwendo wa jioni, na wikendi. Pia, mwishoni mwa mwezi mauzo huwa ya kuridhisha.