Makala

RIZIKI NA MAARIFA: Ameunda ‘Israel ndogo’ mtaani kupitia uvunaji maji na ukulima

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KUSINI Mashariki mwa Bahari ya Mediterranean na Kaskazini mwa Bahari ya Shamu, Israel ni taifa kame ambalo ni kitovu cha kilimomseto, Asia Magharibi.

Kufuatia uongozi bora nchini humo, sheria na kanuni mahususi zimewekwa kuhakikisha hakuna tone la maji linalopotea.

Ikizingatiwa kuwa ni taifa kame, mvua inaponyea, uvunaji wa maji umepewa kipau mbele.

Israel ni mzalishaji mkuu wa matunda na mboga, mazao yanayouzwa maeneo tofauti ulimwenguni.

Pia, ni tajika katika ukuzaji wa ngano, mtama na mahindi. Nchi hiyo imekumbatia mfumo wa unyunyiziaji maji mashamba kwa mifereji.

Historia ya waliokumbatia mfumo huo nchini Kenya ili kufanya kilimo ikiandikiwa hii leo, jina la Timothy Mburu halitakosa kwenye orodha.

Akiwa mzaliwa wa Kaunti ya Nyeri, Mburu anasikitishwa na suala la maji kupotea hususan msimu wa mvua.

Mkulima huyu ameiga mkondo wa nchi ya Israel, ambayo ni jangwa na inayovuna tone lolote la maji, mvua inyeapo.

Kijiji cha Gitinga, Naromoru eneo bunge la Kieni, Nyeri, ni miongoni mwa maeneo kame na yanayopokea mvua kidogo.

Lakini katika shamba la mkulima Mburu, ni kiunga cha kilimo.

Katika shamba lenye ukubwa wa ekari nne, Mburu anakuza mseto wa mimea.

Ana bwawa lenye urefu wa futi 25 kuenda chini na linalositiri zaidi ya lita milioni 40 ya maji.

Limekalia katika kipande cha ardhi chenye ukubwa wa nusu ekari, ingawa maji yako kwenye robo ekari.

Kiini chake cha maji ni msimu wa mvua, ambapo mtaro wenye kimo cha karibu mita 500 urefu na futi 2 kuenda chini umeelekezwa bwawani.

“Kieni ni eneo kame, lakini uvunaji wa maji umegeuza shamba langu kuwa uga wa zaraa,” asema Mburu, akiongeza kuwa shamba lake halikosi mavuno kila mwezi. Mlima Kenya ni kiini cha mito inayoelekeza maji yake Mto Tana, na mkulima huyu anasema kilichomuatua moyo awali ni kuona maji yakipotea.

Mkondo wa Mto Tana humiminia maji yake Bahari Hindi. “Kwa nini maji hayo yapotee ilhali yamepitia kaunti kadhaa, zingine zinazoshuhudia ukame na kukumbwa na njaa?” ashangaa Mburu.

Ni wazo lililomsumbua tangu 2002 hadi 2004, wakati akisomea Stashahada ya Masuala ya Mazingira na Kilimomseto, katika chuo kimoja nchini.

Licha ya kupata ajira, mkulima huyu wa aina yake anasema shabaha yake ilikuwa kutathmini jinsi maji yaliyotoka Mlima Kenya pamoja na ya msimu wa mvua yatavunwa. Mchakato wa uvunaji maji ulianza 2008 ambapo aliibuka na kampeni ‘tone la maji liwajibikiwe’ iliyolenga kuteka maji msimu wa mvua na mito ambayo kiini chake ni Mlima Kenya.

Mburu anasema aliandikia Ubalozi wa Marekani pendekezo la uvunaji maji, na hata ingawa hakupata udhamini lilipitishwa.

“Mwaka 2010 niliandika mapendekezo kadhaa kwa mashirika mbalimbali ya serikali na wadau husika ili kufanikisha wazo langu,” aeleza.

Mashirika aliyolenga ni; Halmashauri ya Kitaifa ya Mazingira-Nema, Warma, Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini – KWS na idara ya kilimo Kieni. Mkulima huyu anasema haikuwa rahisi kushawishi Nema kuhusu uchimbaji bwawa.

Mwaka mmoja baadaye, 2011, shamba lake lilipigwa msasa na akaruhusiwa kulichimba. Hatua ya kwanza ikawa kutafuta mwanakandarasi, ambapo bajeti ya shughuli zote ilitajwa kuwa kima cha Sh1.2 milioni.

“Niliweza kukusanya jumla ya Sh80,000 kutoka kwa mauzo ya mazao niliyokuza kupitia kilimo cha maji ya mvua, kuuza ng’ombe, mbuzi, vifaa vyenye thamani vya nyumba na hata nguo,” adokeza.

Kupitia idara ya kilimo alipata mdhamini aliyempiga jeki kwa mkopo wa Sh400,000.

“Pia ni kupitia idara hiyohiyo ambapo nilipata mdhamini mwingine aliyenikwamua kwa mkopo kuafikia Sh720,000 zilizosalia kufanikisha uchimbaji wa bwawa,” asema.

Aidha, bwawa lilichimbwa kwa trekta kwa muda wa siku 26. Ameliundia ukuta dhabiti na kulizingira kwa ua wa nyaya.

Mburu anasema mnamo 2012 aligura kazi aliyoajiriwa ili kuzamia kilimo kikamilifu. Anafichua kwamba ilimgharimu Sh800 kununua mbegu za viazi.

Shughuli za kuandaa shamba, upanzi na matunzo ndiye alijifanyia mwenyewe.

“Nilianza kwa thumni ekari. Mavuno, nilipata magunia 10 yenye uzito wa kilo 110 kila gunia, moja likinunuliwa Sh6, 000,” afafanua.