Makala

RIZIKI: Ni mpishi hodari na mwanamitindo

March 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kuhitimu mafunzo ya upishi na huduma za mikahawa katika chuo kimoja jijini Nairobi 2013, Anastacia Wangui alipata nafasi ya kazi katika nchi za nje.

Wakati huo alikuwa angali mdogo kiumri, na alitua Dubai, mji wa ufalme katika Shirikisho la Falme za Kiarabu (UAE), ambako alihudumu kama mpishi.

Katika umri huo, hakuwa na mengi, akisema mapato yake aliyaelekeza kwa matumizi yake binafsi. Ni gange anayoisifia kumuingizia mapato ya kuridhisha.

Hata hivyo, alichokosa ni wa kumuelekeza namna ya kujipanga. Mkataba wa kandarasi aliyotia saini, ulipokamilika miaka miwili baadaye, Wangui anasema fedha alizoweka kama akiba zilikuwa haba mno zikilinganishwa na mshahara aliopata.

“Nililazimika kuongeza muda wa kandarasi ili nijipange barabara, ndiposa nikirejea nchini niweze kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo itakayonifaa siku za usoni,” Wangui anasimulia. Miaka ilisonga, na kandarasi ikatamatika bila kufanya maendeleo aliyopania.

Ni hali inayoshuhudiwa na kuzingira vijana wengi, hasa wanapokosa mshauri. Katika mukhtadha huo, Elvis Kiptoo, mhasibu na mtaalamu wa masuala ya fedha, anasema muhimu zaidi ni kuwa na mikakati maalum jinsi ya kuwekeza.

“Kuna mashirika ya kifedha, unayoweza kufungua akaunti unaelekeza mapato yako humo. Baadhi wamefanikisha kununua vipande vya ploti wamejenga nyumba za kupangisha ikiwa ni pamoja na mashamba makubwa wakiendelea kufanya kazi ughaibuni,” Kiptoo ashauri, akieleza kwamba akiba unayoweka unapaswa kuitumia kupiga jeki mapato yako kwa kuwekeza kwenye miradi inayoingiza faida.

Mdau huyo hata hivyo anaonya wanaotumia watu wa familia fedha wanazopata wawafanyie miradi, akisema wengi wamepata miradi hewa.

“Hifadhi pesa zako kwenye mashirika ya kifedha kama vile benki na vyama vya ushirika ndivyo Sacco,” anahimiza mtaalamu huyo.

Katika kisa cha Anastacia Wangui, anasema alirejea nchini na alichoweza kununua ni vifaa chache vya mapishi pekee. Kulingana naye, vifaa hivyo visingetosha kuanzisha kazi aliyolenga ya mapishi tamba.

Hakuwa na budi ila kutafuta ajira nchini kuafikia malengo yake. Ukosefu wa kazi nchini hususan miongoni mwa vijana ni donda ndugu. Wangui anasema alibisha milango ya hoteli mbalimbali jijini Nairobi kwa miezi kadhaa bila mafanikio.

Alipata vibarua vya siku moja, mbili, tatu na ambavyo malipo yake ni ya chini.

Ni kupitia rafikiye alipata mwaliko kama mpishi nchini Uhabeshi, ambapo alienda humo 2018 na kufanya kazi hiyo hadi mwanzoni mwa 2019.

“Hata ingawa mapato hayakuwa ya kuridhisha vile, nilitumia fursa hiyo ya kipekee kujipanga,” anaeleza.

Anastacia kwa sasa anafanya huduma za mapishi tamba, ambapo hupokea mialiko ya hafla kama vile harusi, utoaji mahari, kwenye makanisa, miongoni mwa hafla zingine zinazohitaji huduma hizo.

Mwandalizi, humtabiria idadi ya watu anaotarajia, Wangui anaandaa bajeti ya mahitaji ikiwa ni pamoja na ada ya leba. Ana kundi la wahudumu ambao wamesomea mapishi na vilevile kuwahudumia wateja.

Mpishi huyo hodari na wa aina yake anasema hafla husheheni wakati wa likizo; mwezi Aprili, Agosti na kilele kikiwa msimu wa Krismasi mwezi Desemba. Mialiko mingi huwa wikendi, ambapo hafla huandaliwa.

Hakuna barabara isiyokosa milima na mabonde, mwezi Januari, Februari hadi Machi, anasema hafla huwa finyu mno, jambo linalomlazimu nyakati zingine kukaa bila kazi. Kwenye mipango yake, katika ruwaza ya miaka michache ijayo, anapania kununua tanuri, jiko maalum la kuoka keki na mikate. “Ninapanga kufungua duka la kuoka keki, nikilenga wanaofanya harusi na wanaothamini na kuadhimisha siku zao za kuzaliwa, za wanao na hata marafiki,” afafanua, akisema ni mpango unaohitaji kitita kikubwa cha pesa.

Kando na kuwa mpishi, Wangui ni mwanamitindo. Aidha, anathamini mavazi yenye asili ya Kiafrika, hasa suti za wanawake, hayo yakijumuisha suruali ndefu na sketi.