RIZIKI: Ni mwendeshaji bodaboda aliyeacha kazi ya mama-mboga
Na PHYLLIS MUSASIA
KWA miaka mingi, Brenda Mbalilwa aliuza mboga lakini mapato kutokana na biashara hiyo hayakutosheleza mahitaji ya familia yake.
Na hali ilipozidi kuwa ngumu mahitaji yakiendelea kuongezeka, Brenda mwenye umri wa miaka 30 aliamua kujaribu bahati katika sekta ya uchukuzi wa bodaboda ili kuongeza kipato.
Mwaka wa 2017, aliikacha biashara ya mboga na kujitosa katika uendeshaji wa bodaboda mjini Nakuru.
“Nilifanya bidii na kuwekeza fedha katika chama kimoja na baadaye akiba hiyo ilipozidi, niliruhusiwa kuchukua mkopo wa Sh140,000 ulioniwezesha kununua pikipiki ambayo sasa natumia kwa kazi yangu,” Brenda anaambia Taifa Leo.
Alianza kwa kuwaajiri vijana wawili lakini walionekana kucheza na kazi.
“Kulikuwepo na makubaliano ya fedha na utaratibu wa kazi na watu hao lakini wote wawili walifanya kazi kinyume na tulivyoelewana,” akasema.
Kulingana naye, alihitajika kulipa mkopo aliochukua chamani na pia kuongeza mapato yake ya kila siku; jambo lililomsukuma kuchukua jukumu la kuendesha bodaboda yake mwenyewe.
“Nilizaliwa Magharibi mwa Kenya na nikalelewa katika familia ambayo kila mmoja wetu alizoea kutumia baiskeli katika shughuli mbalimbali. Sikupata shida yoyote wakati wa kufanya kazi ya bodaboda kwa sababu ya uzoefu wa kuendesha baiskeli,” akaongeza.
Ilimchukua muda mchache kujifunza kuendesha pikipiki hata kabla anunue hii yake. Wakati huo hakujua angefanya kazi ya bodaboda.
Mama huyo wa watoto watatu anasema haikuwa rahisi kwa mumewe kumruhusu kubadili kazi na kuanza kuendesha bodaboda.
“Mara ya kwanza hakuniruhusu nifanye kazi hii kwa sababu aliona kwamba ni kazi ngumu kwangu na pia itaniweka katika hali hatari barabarani na hata kuyumbisha ndoa yetu,” akasema na kubainisha mume aliona tatizo la kuwalinda watoto.
Brenda alizungumza na babake mzazi ambaye naye alifanya mazungumzo na mumewe ndipo akamruhusu kuanza kazi hiyo.
“Babangu alinielewa na hakuwa na tatizo lolote,” akasema.
Kabla ya janga la Covid-19, amekuwa anafunga kazi mfukoni akiwa na mapato ya kati ya Sh1,500 na Sh2,000 lakini wakati huu mgumu anapata kati ya Sh600 na Sh700 kwa siku.
“Siwezi kulalamika licha ya kwamba kazi imerudi chini kwa sababu bado nina uwezo wa kununua chakula na mahitaji mengine ya familia yangu. Nimefanya kazi hii kwa muda wa miaka minne sasa na bado ninaendelea,’’ anajipa tumaini.
Licha ya changamoto za hapa na pale, mwanamke huyu mkakamavu anasema atazidi kuifanya kazi ya bodaboda na kwamba hana nia ya kubadili mawazo kuhusiana na kazi hiyo.
Baadhi ya matatizo anayopitia ni pamoja na kunyanyaswa na wateja wenye nia mbaya kama vile kubebwa na kisha kutoweka bila kulipa nauli.
Katika kisa cha hivi maajuzi, Brenda anasikitika jinsi alivyopoteza zaidi ya Sh600 kutoka kwa mteja mmoja ambaye alimpeleka katika sehemu mbalimbali mjini Nakuru.
“Baada ya kusafiri katika sehemu nne tofauti, mteja huyo alistahili kunilipa Sh600 lakini mwishowe alitoweka na nilipomfuata na kumuitisha pesa zangu, aliniambia alikuwa mlevi na kwamba hakukumbuka ikiwa alitumia bodaboda yangu,” akasema.
Changamoto nyingine anasema ni wivu ambao hutokea kwa wanabodaboda wenzake kila mara wateja wanapompendelea.
“Kuna baadhi ya wateja ambao hupendelea kubebwa na mimi kwa sababu wazijuazo wao wenyewe. Hali hii huleta chuki kutoka kwa wenzangu pale steji na nimeishi kuzoea,” anasema.
Anaongeza kuwa changamoto hizo miongoni mwa nyinginezo, zimemsaidia kufanya kazi kwa bidii na kuwa mtu wa kujitegemea.
“Kila mtu yuko mji huu kutafuta shilingi na huwezi kufanya kazi kwa manufaa ya wengine. Kuwa mwanamke mwendeshaji bodaboda kumenifunza kukaa ngumu katika kila jambo kila wakati na ndiyo maana bado naendelea,” akasema.
Mumewe, Bw Amos Obura anamuunga mkono mkewe na siku zote amekuwa akimshauri kutia bidii ili kuimarisha familia yao.
Bw Obura anasema mkewe ana bidii ya mchwa na kila kazi anayoifanya huwa mkakamavu katika malengo yake.
“Kazi ya bodaboda ni kazi ya kawaida na inamsaidia kupata hela kwa matumizi yake binafsi na pia katika kuimarisha familia,” akasema.
Siku za usoni, Brenda analenga kuanza mradi wa kutoa ushauri kwa wanawake katika Kaunti ya Nakuru ili kuwaeleza kuhusu ubora wa kujitolea na kufanya kazi bila kubagua.
Anawashauri kina mama kujitokeza na kufanya kazi zote ambazo kwa muda mrefu zimesawiriwa kuwa za wanaume pekee.
“Kama ilivyo katika sekta ya usalama na ulinzi, wapo maafisa wa kike katika jeshi la nchi kavu, wanamaji na ulinzi wa mipaka ya nchi. Wapo pia kina mama katika kazi nyinginezo kama vile uhandisi wa barabara ambapo si tofauti sana na kazi hii ya bodaboda,” akashauri.