• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
RIZIKI: Utamu wa kuuza miwa

RIZIKI: Utamu wa kuuza miwa

Na SAMMY WAWERU

BARABARA kuu ya Thika Superhighway, inayounganisha ni yenye shughuli chungu nzima kila sekunde na dakika katika usafiri na uchukuzi.

Pembezoni, baadhi ya wananchi wamejituma kujiendeleza kimaisha, na kuimarisha uchumi, la mno likiwa kujitafutia riziki halali.

Bw Isaac Muhuthu ama toroli iliyopakiwa miwa, kifaa cha kuzichambua na mifuko ya kupakia.

Ni kazi anayosema ameifanya kwa zaidi ya miaka mitano na haijutii kamwe.

“Uuzaji wa miwa ndiyo ofisi yangu. Ninakimu familia yangu kupitia gange hii,” Bw Muhuthu anaambia Taifa Leo.

Kijana huyu ni mmoja wa waliojituma kufanya biashara, ikizingatiwa kuwa nafasi za ajira Kenya hasa kwa vijana ni finyu mno. Licha ya serikali ya Jubilee kuahidi kuwa itakuwa ikibuni nafasi milioni moja kila mwaka, hilo lingali kitendawili.

Kulingana na Muhuthu, vijana hawana budi ila kuweka vyeti vyao vya masomo kando na kuingilia biashara au shughuli zozote halali zinazoingiza mapato kama vile kilimo, ima fa ima gurudumu la maisha lazima lisukumwe.

Kwa mwaka maelfu ya vijana hufuzu kwa vyeti vya masomo kutoka taasisi mbalimbali za juu za elimu. “Almuradi kazi ni halali, vijana waifanye. Ajira za ofisi hazipatikani, wanakowekeza wazifanye afisi zao,” aeleza Muhuthu.

Kulingana na mjasirimali huyo ilimgharimu mtaji wa Sh7,000 kuanzisha biashara ya uuzaji wa miwa.

“Nilinunua toroli Sh5,000 na miwa Sh2,000 na kazi ikaanza,” anasema.

Huuza kwa kuchuuza, katika vipitio vya watu pembezoni mwa Thika Superhighway.

Anasema muwa huuziwa Sh35 kutoka kwenye maghala, wafanyabiashara wanaonunua kwa kijumla kuuzia wale wa wastani na wale wadogowadogo.

“Mmoja hunipa faida kati ya Sh15 na Sh65,” anafichua.

Kwa mujibu wa maelezo yake, wakati kazi imenoga hususan miale ya jua inapoangaza, huuza hadi miwa 70 kwa siku.

Hakuna kazi isiyokosa pandashuka, baridi hushusha mauzo.

“Msimu wa mvua au baridi, watu hawali miwa kwa wingi,” anadokeza.

Ili kuimarisha biashara yake, mhasibu na mtaalamu wa masuala ya kiuchumi Dennis Muchiri anamshauri kuwekeza katika uongezaji wa thamani kwa miwa.

Bw Muchiri anasema anapaswa kuweka akiba kununua mashine ya shughuli hiyo.

“Kuna sharubati inayotengenezwa kwa miwa, na inaweza kuhifadhika kwa muda akitafuta soko la bidhaa zake,” amhimiza.

Pia huchanganywa kwa matunda ainati, ili kuongeza ladha na madini faafu kwa mnywaji. Hata ingawa ni uwekezaji unaohitaji fedha za kutosha, Muchiri anasema aweke akiba polepole kwa sababu ya siku za usoni.

“Utengenezaji wa sharubati ya miwa na matunda kwa njia nyingine ni kiwanda, na ni mojawapo ya ajenda kuu ya uimarishaji wa viwanda nchini anayolenga Rais Uhuru Kenyatta,” anafafanua mdau huyo.

Kimsingi, juisi ya miwa ni sukari halisia, ambayo haijachakatwa. Ni nzuri kwa mwili kwa sababu virutubisho na madini mengi.

Wataalamu wa afya wanasema ina uwezo wa kuupa mwili nguvu kwa sababu ya ‘glucose’ iliyopo. Pia, ina kalori na vitamini.

Madini halisi yaliyoko kwenye sukari ya miwa ni kama Phosphorus, Calcium, madini ya Chuma na Potassium.

Si hayo tu, miwa ni jamii ya mimea yenye alkali hivyo basi ina uwezo wa kupambana na Saratani hasa ile ya kibofu cha mkojo na ya matiti.

Isitoshe, miwa ina upekee wake kwani ina uwezo wa kuongeza maji mwilini na kuupa nguvu.

You can share this post!

Gavana Awiti ‘awapoteza’ maseneta kwa...

Utata na ubovu wa ukumbi wa umma Eastleigh

adminleo