Roboti inayojiendesha kuboresha kilimo
HUKU ulimwengu ukipambana kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi, sekta ya kilimo haina budi ila kutathmini utendakazi wake ili iwe endelevu.
Ukumbatiaji wa teknolojia za kisasa, ni kati ya mikondo itakayookoa shughuli za kilimo.
Bunifu kuboresha kilimo na teknolojia kama vile AI, zinatajwa kuwa katika mstari wa mbele.
Matumizi ya droni yanashabikiwa kuleta mchango kukabiliana na athari za tabianchi, watafiti sasa wakijumuisha roboti kwenye mtandao huo.
Chuo Kikuu cha Kilimo na Masuala ya Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kwa ushirikiano na wadauhusika kimekuwa kikiunda mashine na mitambo ya kilimo inayoweza kutoa huduma shambani, roboti ikiwemo.
Taasisi hiyo ya elimu ya juu, imeashiria kupata nuru kwenye jitihada zake.
Kupitia Mpango wa Mafunzo ya Roboti, unaojulikana kama Robotics Dojo, wanafunzi wa taasisi hiyo wameonyesha umahiri kwenye bunifu za kilimo na roboti inateka mawazo ya wengi.
Mpango huo ni kati ya mradi wa AFRICA-ai-JAPAN, unaolenga kuboresha vipaji katika utafiti.
Kwenye mashindano ya Oktoba 2024 yaliyoleta pamoja wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali hususan vinavyotoa mafunzo ya kilimo na utafiti, wale wa JKUAT walizindua roboti yenye sensa.
Aidha, roboti hiyo inaweza kutambua mahitaji ya mimea shambani na kuangazia changamoto.
Kulingana na Dkt Shohei Aoki, Mratibu wa Mpango wa Robotic Dojo JKUAT, utendakazi wa roboti hiyo utasaidia kutatua changamoto zinazochochewa na tabianchi.
Isitoshe, mtambo huo utafaa zaidi taifa katika kufanikisha ajenda ya uzalishaji wa chakula cha kutosha na pia kuangazia leba.
“Itakuwa afueni kwa wakulima; kuwasaidia kupunguza matumizi ya dawa zenye kemikali kwa sababu changamoto za mimea zitatambuliwa mapema kupitia roboti, na vilevile kupunguza upotevu wa mimea,” Dkt Aoki akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano JKUAT.
Ilivyoundwa, mtafiti huyo alisema sensa zake zina uwezo kutambua mahitaji ya mimea shambani, hulka muhimu sana katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yatasaidia mkulima kudhibiti matumizi ya maji, mbolea, kemikali, hivyo basi kupunguza upotevu wa pembejeo na kufanikisha kilimo endelevu.
Ni roboti inayojiendesha na kujitegemea kutoa huduma, kwa lugha ya Kiingereza autonomous robot.
“Roboti zilizo na uwezo kujiendesha zinaweza kubadilisha sekta ya kilimo,” Aoki anasema.
Dkt Aoki, ambaye ni mtaalamu wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), amekuwa akisaidia JKUAT katika masuala ya utafiti wa kilimo.
Mashindano ya Robotics Dojo, ambayo 2024 yalitinga Makala ya Tatu, yalizinduliwa 2022, yakiwa na lengo kuinua utafiti wa roboti kuboresha sekta ya kilimo na viwanda.
Ya mwaka huu, 2024, yalilenga roboti zinazojiendesha kwa kutumia teknolojia ya Simultaneous Localization and Mapping (SLAM), ambayo huruhusu roboti kusafiri katika mazingira yasiyojulikana kwa kutumia sensa za miale ya laser (lidar).
Wanafunzi walioshiriki kuunda mtambo huo, kila mmoja alipewa bajeti ya Sh20, 000 kutengeneza.
“Roboti zinazojiendesha zinaweza kunyunyizia mimea dawa dhidi ya wadudu na kwekwe, kwa mujibu wa athari zinazojitokeza, hivyo basi kudhibiti matumizi ya kemikali na kulinda mazingira,” Dkt Aoki anafafanua.
Roboti hiyo ikiboreshwa, inaweza kutumika kufanya mavuno, hivyo kuwa na manufaa tele kwa mkulima kwani itapunguza kazi za mikono.
Tangu kuzinduliwa kwake miaka mitatu iliyopita, Mpango wa Robotics Dojo umetoa mafunzo kwa wanafunzi 146 kuhusu roboti.
Makala ya 2024, yalishirikisha wahusika 41 kutoka JKUAT, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Dedan Kimathi (DeKUT) na Pan African University Institute for Basic Sciences, Technology, and Innovation (PAUSTI).
Mohamed Ibrahim, mwanafunzi wa mwaka wa nne JKUAT kozi ya Uhandisi wa Kieletroniki na Kompyuta, aliongoza kikosi chake katika kutafiti utengenezaji wa roboti inayojiendesha.
“Mashindano kama haya yanahamasisha ubunifu na kuwapa wanafunzi jukwaa kulinganisha ujuzi wao na wa wenzao, na pia kusaidia kuleta suluhu katika sekta ya kilimo, viwanda na usafiri,” Ibrahim akasema.
Akisisitiza umuhimu wa roboti katika kuangazia changamoto kuu kama uhaba wa wafanyakazi shambani na ukosefu wa raslimali, mtafiti huyo mchanga alieleza uwezo wa teknolojia ya matumizi ya sensa za miale ya laser (lidar) kubadilisha sekta ya kilimo, ili ihimili mikumbo ya tabianchi.
JKUAT, taasisi inayojulikana kwa mafunzo ya kilimo na teknolojia, inalenga kuhamasisha matumizi ya roboti kupanda mimea, kuinyunyizia dawa na pia kufanya mavuno.