Makala

Ruto atekeleza vitisho, apokonya magavana Sh10 bilioni za barabara

Na  Dominic Omondi May 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ametekeleza vitisho vyake vya kutwaa fedha za ujenzi na ukarabati wa barabara, ambazo zimekuwa chanzo cha mvutano mkubwa kati ya serikali za kaunti na wabunge, kwa kuanzisha kifungu kipya cha matumizi katika bajeti ya serikali kuu kinachoitwa kazi za barabara.

Makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha unaoanza Julai, yaliyowasilishwa bungeni na Hazina ya Taifa, yanaonyesha kuwa Sh11.47 bilioni zimetengewa Idara ya Barabara chini ya serikali kuu.

Sehemu kubwa ya fedha hizo zitaelekezwa katika ujenzi wa barabara za mashambani na vijijini,ambazo zimekuwa chanzo cha mvutano kati ya kaunti na wabunge.

Katika hatua ambayo inaweza kuchochea vita vipya vya kisiasa, serikali kuu imetwaa baadhi ya miradi ambayo serikali za kaunti zilikuwa tayari zimeanzisha. Hii ni katika muktadha wa mvutano unaoendelea kuhusu usimamizi wa hazina ya Sh10 bilioni za Hazina ya Ukarabati wa Barabara (RMLF).

Hatua hii inaonyesha dhamira ya serikali ya Ruto, ambayo hadi sasa haijazindua mradi mkubwa wa barabara kama ilivyofanya serikali iliyopita kusimamia pesa hizi.

Serikali ya Ruto inakumbwa na mzigo mkubwa wa madeni, jambo linaloifanya ishindwe kukopa fedha za miradi mikubwa kama ya mtangulizi wake.

Kifungu hiki kipya cha bajeti cha “Kazi za Barabara” pia kitaelekeza fedha kwa miradi ya barabara, hasa katika maeneo ya Luo Nyanza — ngome ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga — ambaye alimuunga mkono Rais Ruto mwaka jana wakati wa maandamano ya kupinga ushuru.

Ikiwa imebaki miaka miwili kuelekea uchaguzi wa 2027, Rais Ruto anaonekana kutaka kurithi kura zote za Luo Nyanza endapo chama cha ODM cha Odinga hakitawasilisha mgombea wa urais, na badala yake kumuunga mkono Ruto kwa muhula wa pili.

Hii ndiyo sababu baadhi ya maeneo yatakayonufaika ni Suba Kusini, Nyatike na Ndhiwa, kila moja ikitengewa Sh100 milioni.Maeneo mengine ni eneobunge la Kieni na Kaunti ya Mandera, pia kila moja Sh100 milioni.

Katika Kaunti ya Migori, serikali ya Ruto itachukua mradi wa kuboresha barabara ya Tella–Gogo hadi kiwango cha lami. Mradi huu ambao ulikuwa umefadhiliwa na Idara ya Barabara ya Kaunti ya Migori umetengewa Sh100 milioni.

Kaunti ya Migori pia ilikuwa imetoa Sh9.7 milioni kwa ukarabati wa barabara ya Kanyawanga–Dede–Rapogi, lakini sasa serikali kuu imetenga Sh300 milioni kuiwekea lami.Hapo awali, zabuni ya kuiboresha barabara hiyo ilikuwa chini ya asilimia 10 ya fedha za RMLF kupitia Mamlaka ya Barabara za Vijijini (KeRRA).

Katika Kaunti ya Siaya, barabara ya Wangarot–Asembo Bay–Kalendiu imetengewa Sh100 milioni. Aidha, serikali kuu imetenga Sh200 milioni kuboresha barabara ya Sidindi–Sigomere–Masiro.

Barabara hizi zilikuwa zimepangwa kufadhiliwa na serikali ya kaunti ya Siaya, lakini sasa zimo katika bajeti ya serikali kuu.Rais Ruto amekuwa akisema wazi kuwa anataka kuchukua usimamizi wa hazina hiyo, akiwakosoa wabunge na serikali za kaunti kwa matumizi mabaya ya fedha za RMLF.

“Naomba waheshimiwa wabunge—najua kuna mvutano unaoendelea kati ya kaunti na Bunge kuhusu fedha za ukarabati wa barabara,” alisema Rais wakati wa ibada ya Pasaka Ntulele, Kaunti ya Narok.

“Mkiniachia mimi, nitahakikisha miradi hii yote inatekelezwa ipasavyo. Kwa sababu sasa hivi mnajenga barabara za mchanga fupi, lakini mvua ikinyesha mara moja zinaharibika,” aliongeza.

Raila Odinga pia amejiunga na mjadala huo, akipendekeza kuvunjwa kwa KeRRA na KURA, na kaunti kuachiwa majukumu ya miradi ya barabara.